Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Mhe . Nickson John Simon amekabidhi rasmi ofisi ya Wilaya ya Kibaha kwa Mhe. Fadhil Nkurlu ambaye ameteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kushika nafasi hiyo baada ya kukamilisha mchakato wa kuteua wakuu wa wilaya nchini.
Makabidhiano hayo yamefanyika leo Oktoba 02, 2026 na kuhudhuriwa na viongozi wa ngazi mbalimbali wa Idara za Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha, viongozi wa chama na wa taasisi zilizopo ndani ya Wilaya hiyo.
Akizungumza wakati akikabidhi ofisi hiyo Mhe. Nickson ambaye amehamishiwa Wilaya ya Songwe Mkoani Songwe, amesema anaondoka Kibaha akiwa ameacha kumbukumbu nzuri ya kusimamia na kukusanya mapato ya ndani kwa Halmashauri mbili ambazo ni Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha na Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Vijijini.
Amesema, ameondoka Kibaha kiutendaji na kiutumishi lakini moyo wake umejaa upendo mkubwa wa wana Kibaha ambao walimpokea , kumleta na kumfunda hadi kuendelea kuaminiwa tena na Rais Samia, hivyo kwake watabaki kuwa watu muhimu kwenye historia ya maisha yake.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya Kibaha, Mhe. Fadhil Nkurlu akizungumza baada ya kukabidhiwa ofisi hiyo, amesema amewaambia viongozi wa Wilaya hiyo na wananchi jambo kubwa ni kuendelea kushirikiana kwa lengo moja tu la kuleta maendeleo.
Mhe. Nkurlu amesema kikubwa ni kuendelea kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM, lakini kubwa zaidi wote kwa umoja wao watasonga mbele.
Hivyo amesisitiza maono yake kwa Kibaha ni kuendelea pale alipoishia Mkuu wa Wilaya aliyepita na anategemea kupata ushirikiano atakaoupata kutoka kwa viongozi mbalimbali wa chama na idara za Halmashauri zote mbili.
Kwa upande wake Naibu Mstahiki Meya Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Mhe. Aziza Mruma amesema anamkaribisha Mhe. Nkurlu na kumuahidi ushirikiano kutoka kwa Baraza la madiwani katika kusimamia na kutekeleza yale yote yaliyo memandani ya Manispaa ya Kibaha.



