TANGAZO

TANGAZO

WMA YALENGA KULINDA HAKI ZA WALAJI NA KUINUA BIDHAA ZA NDANI


Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) imepanga kuimarisha ukaguzi na uhakiki wa vifaa vya vipimo vinavyotumika viwandani na katika biashara, ili kulinda haki za walaji, kuongeza ubora wa bidhaa zinazozalishwa nchini na kuimarisha ushindani wa wazalishaji wa ndani katika masoko ya kimataifa.

Hatua hiyo pia inalenga kuhakikisha viwanda na wajasiriamali wadogo na wa kati wanazingatia vipimo sahihi katika kupokea malighafi, uzalishaji na ufungashaji wa bidhaa, ili kuondoa mianya ya udanganyifu na kujenga imani kati ya wauzaji na wanunuzi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Sera ya Maendeleo ya Viwanda ya mwaka 2025 pamoja na sera inayohusu wajasiriamali wadogo na wa kati, Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Alban Kihulla, amesema wakala itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria ya Vipimo, Sura ya 340.

Amesema matumizi ya vipimo sahihi ni msingi muhimu katika kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa na kuuzwa nchini zinakidhi matakwa ya kisheria, huku mlaji akipata kiasi halisi cha bidhaa anacholipia.

Kihulla amesema katika utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Viwanda, WMA itaongeza ushirikiano na viwanda kuhakikisha vifaa vyote vinavyotumika kupimia malighafi na bidhaa katika hatua mbalimbali za uzalishaji vinakaguliwa na kuhakikiwa kwa mujibu wa sheria.

Alivitaja vifaa vinavyohitaji uangalizi huo kuwa ni mizani mikubwa inayotumika kupimia malighafi, vifaa vya kupimia mafuta pamoja na pampu za mafuta zinazotumika katika shughuli mbalimbali za viwandani.

Aliongeza kuwa WMA itaendelea kukagua bidhaa zilizofungashwa ili kuhakikisha uzito au ujazo ulioandikwa kwenye vifungashio unaendana na kiasi halisi kilichomo ndani ya bidhaa husika.

Aidha, bidhaa zinazouzwa kwa kuzingatia urefu na vipimo vingine vya kimaumbile zitafanyiwa ukaguzi ili kuhakikisha zinakidhi matakwa ya kisheria.

Katika upande wa wajasiriamali wadogo na wa kati, Kihulla amesema WMA itaendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kutumia vifaa vya vipimo vilivyokaguliwa na kuhakikiwa kisheria.

Amesema baadhi ya wajasiriamali hukumbana na changamoto katika biashara zao kutokana na kutumia mizani na vifaa vingine ambavyo havijafanyiwa uhakiki, hali inayoweza kuathiri uaminifu wa wateja na ushindani wa bidhaa zao sokoni.

Alisisitiza kuwa wajasiriamali wanaotumia mizani, vipimo vya ujazo na urefu wanapaswa kuhakikisha vifaa hivyo vinakidhi matakwa ya Sheria ya Vipimo.

Vilevile, alieleza umuhimu wa kufungasha bidhaa kwa kuzingatia taratibu zinazotakiwa na kuweka taarifa sahihi za vipimo kwenye vifungashio, ikiwemo uzito unaopimwa kwa kilogramu au gramu, kulingana na aina ya bidhaa.

Kwa mujibu wa WMA, kuzingatia vipimo sahihi kunasaidia kujenga uaminifu wa wateja, kulinda haki za walaji na kuongeza uwezekano wa bidhaa za Tanzania kukubalika katika masoko mbalimbali.

Katika hatua nyingine, Kihulla amesema WMA itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali, zikiwemo Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), katika kuwawezesha vijana na wajasiriamali wadogo.

Amesema ushirikiano huo unalenga kuunganisha ujuzi na uwezo wa vijana katika kubuni na kuzalisha vifaa mbalimbali vya vipimo nchini, badala ya kutegemea kwa kiwango kikubwa vifaa vinavyoagizwa kutoka nje.

Alieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kukuza ubunifu, kuongeza fursa za uzalishaji wa ndani na kujenga uwezo wa vijana kushiriki katika maendeleo ya sekta ya viwanda.