Zikiwa zimepita siku chache toka Shule kufunguliwe Wenyeviti wa Mitaa, Kata ya Hasanga wakishirikiana na Watendaji wa Kata hiyo wametakiwa kusimamia na kufuatilia wanafunzi waliochaguliwa wanaandikishwa Shule ili waweze kupata haki yao ya msingi ya elimu.
Hayo yalisemwa Januari 20, 2025 na Polisi Kata ya Hasanga Sajenti wa Polisi Omar Mustapha katika kikao na Viongozi wa Kata hiyo kilichofanyika katika Ofisi ya Mtendaji wa Kata hiyo iliyopo Mtaa wa Hasanga Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe.
Sajenti Omar aliwataka Viongozi hao kufuatilia watoto wote waliochaguliwa na kujiunga kidato cha kwanza 2025 waanze masomo mara moja na kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kwa wale wazazi ambao wamewapangia majukumu mengine ya kijamii watoto hao ili kuwakatisha ndoto zao na wasitimize malengo yao.
Sambamba na hilo Sajenti Omar aliwataka Viongozi hao kuwahamasisha wananchi ili kuunda vikundi vya ulinzi shirikishi kwani vinasaidia sana katika kuondoa uhalifu na wahalifu katika jamii.
Kwa upande wao Viongozi hao, wamelishukuru Jeshi la Polisi kwa kuendelea kushirikiana nao kwa ukaribu katika mambo ya usalama na wameahidi kulifanya zoezi hilo kwa ukamilifu kwa kufuatilia wanafunzi wote waliofaulu ili waweze kupata haki ya elimu kwa manufaa ya maisha yao na taifa kwa ujumla.


