
-Asema Rais Dkt. Samia amedhamiria kutekeleza na kukamilisha miradi yote ya kimkakati
-Asema Rais Dkt. Samia ni kiongozi anayeona na kusikiliza matatizo ya watu
-Asema CCM itaendelea kuwahudumia Watanzania kwa weledi na uaminifu mkubwa
-Asisitiza CCM imeleta, inaleta na itaendelea kuleta miradi ya maendeleo
-Asema chama hicho kinasema, kinaahidi na kinatekeleza
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Waziri Mkuu Ndugu Kassim Majaliwa amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni tiba ya maendeleo hivyo watanzania wanapaswa kwenda nae kwani ataifikisha nchi kule kunakotarajiwa.
Amesema kuwa Rais Dkt. Samia ni kiongozi anayeona, kusikiliza na kutatua changamoto za Watanzania kwa ustadi wa hali ya juu na amedhihirisha hilo katika kipindi chake cha uongozi.
Ametoa kauli hiyo (Februari 16, 2025) wakati Mkutano Mkuu Maalum Chama cha Mapinduzi Jimbo la Maswa Mashariki, uliofanyika katika uwanja wa nguzo nane,Maswa mkoani Simiyu.
“Rais Dkt. Samia kwa uwezo wake na maono yake ameonesha anadhamira ya dhati ya kuwatumikia watanzania, wote tumeshuhudia nia yake ya kusimamia utekelezaji wa miradi katika sekta mbalimbali za maendeleo na tumeona namna alivyosimamia kukamilisha miradi yote ya kimkakati”.
Akizungumzia Sekta ya Maji Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi imedhamiria kuhakikisha inatekeleza miradi mikubwa ya maji kutoka katika Maziwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa kunakuwa na upatikanaji wa maji safi na Salama “Mpango wetu ni kuendelea kufikisha huduma ya maji mpaka vitongojini”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa katika sekta ya afya Serikali imeendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kuhakikisha huduma za afya zinaimarishwa na kuwapunguzia adha wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya.
Ameongeza kuwa ili kuhakikisha huduma ya upatikanaji wa Umeme inaimarika nchini, Serikali imeendelea kutekeleza miradi umeme “Tumeshafikisha umeme karibu asilimia 99 kwenye vijiji vyetu, sasa tunakwenda vitongojini”
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa chama hicho kipo imara na kinaendelea kuwahudumia Watanzania
Amesema kuwa kutokana na sera imara zinazotekelezaka za chama hicho, kimeendelea kufikisha huduma na mahitaji muhimu kwa Watanzania
“Chama hichi wakati wote kimesimamia utekekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, kinafikisha huduma ambazo wewe mtanzania kila ukiamka ni lazima uzitumie, chama hiki pia kimeendelea kusimamia amani na utulivu nchini”
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki Stanslaus Nyongo amesema kuwa Wilaya imepokea fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye sekta ya elimu, maji, afya, barabara, umeme na kilimo.
Amesema kuwa kupitia RUWASA, Wilaya hiyo imetekeleza miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 2.68 na ongezeko la upatikanaji wa maji imefikia asilimia 81 kutoka asilimia 74.3 “Katika kijiji cha Ipililo, umetekelezwa mradi wa maji wenye thamani ya shilingi bilioni 1.32”
Amesema kuwa katika sekta ya nishati wamefanikiwa kupokea mradi wa Wakala wa Nishati vijijini wenye thamani ya shilingi bilioni 2.79 ambazo zilitumika kuunganisha umeme katika vijiji vyote 56 na vitongoji 117 jimboni humo.
Kadhalika Mheshimiwa Stanslaus amesema kuwa Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 1.57 kwa ajili ya kuimarisha huduma za afya pamoja na kujenga na kukamilisha miundombinu ya afya.