Serikali imesema haitoingilia Mgogoro unaoendelea kufuatia kuahirishwa kwa mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga, Machi 8, 2025, umebaki mikononi mwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na vyombo vyake, huku serikali ikisisitiza kutokuingilia kati suala hilo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo na Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa, alitoa kauli hiyo leo Machi 16, alipokuwa akijibu swali la mwandishi wa habari kuhusu msimamo wa serikali juu ya kuahirishwa kwa mchezo huo. Akizungumza katika Bandari Kavu ya Kwala, mkoani Pwani, Msigwa alisema:
"Ikitokea TFF wamepeleka suala hilo serikalini basi kwa pamoja tutajadili, ila kwa sasa serikali haina neno kwa kuwa suala lipo kwenye mamlaka zinazohusika."
Mechi hiyo iliahirishwa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) baada ya klabu ya Simba kudai kuzuiwa kufanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kabla ya mchezo, jambo lililopelekea Simba kutangaza kutoshiriki mechi hiyo hadi hatua zichukuliwe dhidi ya waliohusika.
Bodi ya Ligi ilieleza kuwa uamuzi wa kuahirisha mchezo huo ulitokana na matatizo ya kiutawala na usalama yaliyojitokeza kabla ya mchezo.
Kwa sasa, TFF na vyombo vyake vinaendelea kuchunguza suala hilo ili kutoa uamuzi stahiki kwa mujibu wa kanuni na taratibu za mchezo.
