![]() |
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imesema kuwa Serikali itaendelea kuboresha miundombinu iliyomo ndani ya Hifadhi za Taifa ikiwemo ukarabati wa barabara, ili kuhakikisha zinapitika kwa urahisi wakati wote na kuchochea maendeleo ya sekta ya utalii nchini.
Hayo yamesemwa Machi 14, 2025, wakati kamati hiyo ilipotembelea Hifadhi ya Taifa Arusha kwa lengo la kukagua miradi ya maendeleo pamoja na eneo la Nasula lililopo kijiji cha Olkung’wado kata ya Ngarenanyuki Mkoani Arusha ambapo wananchi wa eneo hilo wanatakiwa kuhama kwaajili ya kupisha shughuli za uhifadhi na utalii.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Timotheo Mnzava (Mb) alisema kuwa, hakuna utalii endelevu bila miundombinu imara, hivyo ni wajibu wa wizara kuhakikisha barabara hizi zinakarabatiwa kwa wakati na kwa ubora wa hali ya juu ili kuepusha usumbufu kwa wageni. Uboreshaji wa barabara hizi utaongeza idadi ya watalii na mapato yatokanayo na utalii.
Aidha, kamati hiyo ilitoa pongezi kwa Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na TANAPA kwa utekelezaji mzuri wa miradi hiyo na kutoa wito kwa Wizara kuendelea kufuatilia kwa upande wa Wizara ya Fedha, kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa fedha za kulipa fidia wananchi wanaoishi maeneo ya hifadhi hiyo waweze kuhama ili tija iliyokusudiwa ya kuchukua maeneo yale iweze kupatikana.
Akitoa ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Dunstan Kitandula (Mb) alisema kuwa, Serikali iliidhinisha kiasi shilingi Million 419 kwa ajili ya ukarabati wa barabara za vumbi zenye urefu wa kilomita 16 ndani ya hifadhi hiyo kwa lengo la kuhakikisha kuwa wageni wanaotembelea hifadhi hiyo wanapita bila changamoto ya barabara mbovu na hadi sasa mradi huo umekamilika kwa asilimia 100%.
Kitandula aliongeza “Wizara imejipanga kuhakikisha miundombinu ya hifadhi zetu inaimarika kwa kiwango kinachotakiwa. Tutaendelea kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha pia wananchi wanaohama kutoka maeneo ya hifadhi wanalipwa fidia kwa wakati, hatua ambayo itaimarisha uhifadhi wa maeneo haya na kupunguza migogoro”.
Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa Uhifadhi Steria Ndaga ambaye ni Mkuu wa Kanda ya Kaskazini, alisema kuwa TANAPA itaendelea kuangalia na kusimamia miradi hiyo vizuri ili kuhakikisha kuwa hifadhi zetu zinakuwa salama, endelevu, na zenye manufaa ya kudumu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Ziara hiyo ni muendelezo wa juhudi za kamati hiyo katika kuhakikisha sekta ya maliasili na utalii inasimamiwa kwa ufanisi, huku ikihimiza uwajibikaji, matumizi sahihi ya fedha pamoja na usimamizi mzuri wa miradi ili kuhakikisha mchango wa sekta ya utalii unakuwa na tija kwa Taifa.





