TANGAZO

TANGAZO

SERIKALI YAELEKEZA NAMNA YA KUSHUGHULIKIA MASUALA YA KIUTUMISHI IKIWEMO BARUA ZA AJIRA MPYA



Na. Mwandishi Wetu- Dodoma 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amemuelekeza Katibu Mkuu, UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi kuhakikisha barua za walioshinda usaili na kupangiwa vituo vya kazi zinatolewa kwenye mikoa husika walikofanyia usaili badala ya kuwalazimu kusafiri hadi jijini Dodoma Sekretarieti ya Ajira kufuata barua hizo.

Amesema kitendo cha watumishi hao wapya kupatiwa barua katika mikoa husika kitasaidia  kupunguza gharama, usumbufu  pamoja na muda wanaoutumia kufika hadi Dodoma.

Mhe. Simbachawene ametoa maelekezo hayo leo jijini Dodoma wakati akizinda  Baraza  la Wafanyakazi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Mhe. Simbachawene amefafanua kuwa unaweza ukakuta mwananchi amefaulu usaili Mkoa wa Kigoma anaifuata barua jijini Dodoma halafu pengine kapangiwa tena Mkoa huo huo wa Kigoma au Lindi.

Mhe. Simbachawene amesema hayo ni matumizi mabaya ya rasilimali za nchi, ikiwemo  mwananchi mwenyewe  pamoja na fedha anazotumia.

Hii si sawa kwani tunawasumbua wanachoka hata kabla ya kuanza kazi, tuwahurumie, barua hizo wachukulie kwenye mikoa walikofanyia usaili, tuwaamini Makatibu Tawala wetu, tunaamini wapo wataalam wenye maadili wa kufanya kazi hiyo, hivyo tuwape  dhamana waifanye, Mhe. Simbachawene amesisitiza.

Amesema anatamani kuona kwa mfano mwananchi aliyefanyia usaili katika Mkoa wa Rukwa anaifuata barua yake katika Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa kisha  anakwenda pengine  Kigoma alikopangiwa kazi na sio kwenda Dodoma kwanza.


Kama una Taarifa,Picha, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kwa simu +255 766 166 125 au Email : emmymwaipopo@gmail.com