Wakati dunia ikiendelea kukabiliwa na ongezeko la idadi ya watu huku rasilimali kama vile ardhi, mimea, na wanyamapori wakiendelea kupoteza makazi yao, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limejidhatiti kutoa mafunzo mbalimbali yakiwemo ya uongozi ili kukabiliana na wimbi la uvamizi wa maeneo yaliyohifadhiwa na kuhatarisha uhai wa wanyamapori.
Mafunzo hayo yaliyotolewa kwa Maafisa hao yalilenga kuwajengea ujuzi, maarifa na weledi wa kusimamia rasilimali watu, ukusanyaji wa maduhuli, kupanga mikakati bora ya uhifadhi na kufanya maamuzi sahihi katika kulinda maliasili.
Akifunga mafunzo hayo leo Machi 03, 2025, Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara Massana Mwishawa alisema, “Uongozi si tu mamlaka mnayokabidhiwa leo bali pia ni sanaa ya kushawishi, kuelimisha wafuasi ili waelewe na kwenda kutekeleza majukumu yao kwa usahihi. Pia uongozi ni dhana ya kushirikiana na askari mtakaowaongoza ili kulinda rasilimali za Taifa kwa faida yetu sisi tuliopo na kwa wale watakaokuja baadae.”
Aidha, Kamishna Mwishawa aliongeza, “Mmefundishwa viashiria vya kutambua ugaidi na jinsi ya kukabiliana nao, mkumbuke tunasimamia maeneo makubwa zaidi ya asilimia 10 ya ardhi ya Tanzania na maeneo hayo hayana vyombo vingine vya ulinzi tofauti na sisi, wajibu wetu ni kuhakikisha tunayasimamia vizuri kwa kufanya doria za uhakika na mara kwa mara ili maeneo hayo yasigeuzwe kuwa maficho ya magaidi na wahalifu wengine.”
Vilevile, Kamishna huyo aliwahimiza maafisa hao kuwa wazalendo wa kuipenda nchi yao, kwani kwa kufanya hivyo kutawaongezea morali na ari ya kufanya kazi zao na kuwasimamia wafuasi wao kulinda na kuhifadhi maliasili hizo walizokasimishwa kwa faida ya watanzania wote.
![]() |
Hata hivyo Kamishna Mwishawa aliwatahadharisha maafisa hao kuwa askari asipopangiwa kazi na kupewa maelezo toshelezi, watajipangia kazi wenyewe na ikitokea kazi waliyojipagia wakaharibu na kuwa na makandokando atakayewajibika ni kiongozi aliyeshindwa kutekeleza wajibu wake. Hivyo ni wajibu wa kiongozi kusimamia na kutekeleza wajibu wake ipasavyo.
Mwanamapinduzi wa India aliwahi kusema,”The greatness of a nation and its moral progress can be judged by the way its animals are treated”. Hivyo jukumu la uongozi walilopewa maafisa hao, la kulinda wanyamapori na kuwasimamia askari ambao ni walinzi wakuu wa maliasili hizo ndio itakuwa ni chachu ya kuendekea kuwa na rasilimali hizi au la!
Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Katavi Dkt. Emilian Kiwele akimkaribisha Naibu Kamishna Mwishawa alisema, “Changamoto kubwa ya Uhifadhi ni pamoja na ujangili wa wanyamapori na uingizwaji wa mifugo hifadhini pamoja na upotevu wa maduhuli hivyo kama viongozi wapya mna nguvu za kutosha kwenda kuyasimamia haya kwa faida ya TANAPA na Taifa kwa ujumla”.
Akiongea kwa niaba ya Maafisa wenzake waliopandishwa vyeo leo Afisa Uhifadhi Daraja la Pili Paulina Mkama aliyekuwa Askari Daraja la Kwanza alisema, “Tunaushukuru uongozi wa TANAPA kwa kututunuku vyeo hivyo kulingana na sifa tulizokuwanazo, hii imetuongezea chachu ya kufanya kazi kwa bidii, kwani mafunzo haya yametujengea uzalendo, nidhamu na ujuzi wa kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi wa hali ya juu na tutakuwa ni viongozi bora na sio bora viongozi.”
Hafla ya kufunga mafunzo hayo iliyofanyika leo katika Kituo cha Mafunzo Mlele kilichopo mkoani Katavi imejumuisha maafisa 31 kutoka Idara na vitengo mbalimbali huku wote wakitoa katika Kada ya uaskari baada ya kujiendeleza kimasomo.