Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani (Mst) Mbarouk Salim Mbarouk akizungumza wakati akifunga mafunzo ya siku mbili ya watendaji wa uboreshaji wa Daftari kutoka halmashauri zote za mkoa wa Dar es Salaam leo Machi 07,2025.
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi -INEC imewataka watendaji wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wa Mkoa wa Dar es Salaam kuwahamasisha wananchi wenye sifa ili wajitokeze kujiandikisha na kupata haki yao ya kikatiba itakayowawezesha kushiriki katika kuchagua viongozi wao.
Wito huo umetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufani Mstaafu wa Mahakama ya Rufani MH. MBAROUK SALIM MBAROUK wakati akifunga mafunzo ya siku mbili ya watendaji wa uboreshaji wa Daftari kutoka halmashauri zote za mkoa wa Dar es Salaam.
Sambamba na hayo Makamu Mwenyekiti huyo wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mh Mbarouk Salim Mbarouk amewasisitiza washiriki wa mafunzo kuhakikisha wanahamasisha wananchi kwa kusambaza mabango waliyopewa na Tume.
Amesema mabango hayo yakisambazwa kwenye maeneo yao ya kiutendaji, wananachi watapata taarifa za kina kuhusu zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linalofanyika kwa muda wa siku Saba kuanzia Machi 17 hadi 23, 2025.
Jaji Mbarouk amewaasa kuwa licha ya shughuli nyingi za kiutendaji walizonazo watendaji hao wafuatilie kwa karibu zoezi hilo na kushiriki kikamilifu ili kuhakikisha kuwa linafanikiwa.
Katika hatua nyingine Jaji Mbarouk amewakumbusha watedaji hao kuhusu uwepo wa mawakala wa vyama vya siasa na kuwasisitiza kuhusu umuhimu wa kuwapa ushirikiano kwa sababu ni wadau muhimu.
Naye Mwenyekiti wa Mafunzo amesema siku mbili za mafunzo zimetumika ipasavyo kuhusu Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga uboreshani unaotarajiwa kuanza siku Kumi zijazo.
Mafunzo haya ya nadharia na vitendo yaliyoanza jana na kumalizika leo Machi 7 yalilenga kufundisha namna ya kutumia vifaa vitakavyotumika kwenye zoezi la Uboreshaji la Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ni sehemu ya maandalizi ya uboreshaji wa Daftari hilo mkoani Dar Es Salaam ambao utaanza Machi 17 hadi 23, 2025.






