Na: Happiness Sam - Arusha
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb), ameliagiza Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kuwekeza katika teknolojia kama kamera za kisasa, Ndege Nyuki “Drones”, GPS na mifumo ya kielektroniki ili kuimarisha ulinzi wa hifadhi dhidi ya ujangili na uharibifu wa mazingira.
Akizungumza Machi 29, 2025, katika ziara yake Hifadhi ya Taifa Arusha, alikagua miradi ya maendeleo na kutoa maelekezo ya kuboresha huduma za utalii na uhifadhi wa wanyamapori.
Waziri Chana alisema kuwa matumizi ya teknolojia yatasaidia kuongeza ufanisi wa ulinzi wa wanyamapori na rasilimali za asili katika hifadhi.
Aidha, alipongeza juhudi za Hifadhi ya Taifa Arusha katika kuboresha sekta ya utalii kupitia ukarabati wa miundombinu na ujenzi wa nyumba za kulala wageni.
“Ninaipongeza Hifadhi ya Taifa Arusha kwa kazi nzuri ya kuhifadhi rasilimali za Taifa na kuboresha mazingira ya utalii, ikiwa ni pamoja na ukarabati wa barabara ya kilomita 16 uliogharimu shilingi milioni 419 na ujenzi wa nyumba za kisasa za kulala wageni kwa shilingi milioni 204. Hatua hii inahakikisha wageni wanapata huduma bora,” alisema Waziri Chana.
Pia ameipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi za kukuza sekta ya utalii kupitia filamu ya Royal Tour na Amazing Tanzania, ambazo zimeitangaza Tanzania kimataifa na kuongeza idadi ya watalii.
Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi (TANAPA), Musa Nassoro Kuji, alimshukuru Waziri Chana kwa kutembelea Hifadhi ya Taifa Arusha na kuahidi kutekeleza maagizo yote kwa umakini ili kuendeleza uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya jamii.
Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Eva Malya, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Arusha, alisema hifadhi hiyo itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia vipaumbele vya Taifa, ikiwemo kuboresha miundombinu ili kuwezesha watalii kuvifikia vivutio vya utalii.