Na Mwandishi wetu, Morogoro
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA), Mussa Juma amewaomba viongozi wa vyama vya siasa nchini kuhakikisha wanawawalinda Waandishi Habari katika uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba Mwaka huu.
Mwenyekiti huyo wa Jowuta ametoa wito huo leo Aprili 24 mwaka huu Mkoani Morogoro katika Semina ya kuwajengea uwezo wanachama wake ili kuandika habari za Uchaguzi kwa kufuata misingi ya tasnia.
"Kumekuwa na tabia kadhaa zikitokea hususani katika kipindi cha chaguzi ambapo baadhi ya waandishi wamekuwa wakipitia changamoto nyingi ikiwemo kushushwa kwenye misafara ya vyama vya siasa kutokana na kuandika taarifa kinyume mahitaji ya vyama hivyo.
"Kulingana na changamoto hizo ambazo zimekuwa zikiwaondolea uhuru waandishi, tunaviomba vyama vya siasa wawalinde waandishi ili wawe huru kutumia kalamu yao vizuri bila bugudha, "amesema.
Hata hivyo amewahasa waandishi wa Habari kuandika habari zinazohusisha uchaguzi kwa kufuata misingi ili kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza na kuziweka nchi salama.
Mafunzo hayo ambayo yanaratibiwa na JOWUTA ni ya Awamu ya Kwanza yamefanyika kwa wanachama wao wa kanda ya Dar es Salaam na Pwani na kufuata Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Kaskazini.
Jowuta inatoa mafunzo hayo kwa kushirikiana na Shirikisho la Kimataifa la Waandishi Duniani(IFJ) ambao ndio wadhamini wakuu na wengine ni Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binaadamu(THRDC) ni Shirikisho la Waandishi Afrika(FAJ) na MAIPAC.
Uchaguzi Mkuu nchini Tanzania unafanyika kila baada ya Miaka mitano na unahusisha kumchagua Rais, Wabunge na Madiwani.


