Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza maadhimisho ya sherehe za Muungano za mwaka huu yafanyike katika mikoa yote yakiongozwa na viongozi wakuu wa Serikali.
Ameyasema hayo jana (Jumatano, Aprili 9, 2025) alipowasilisha hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Mtumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2025/2026 Bungeni jijini Dodoma.
”Viongozi hao pamoja na masuala mengine, watajumuika na wananchi katika shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo uzinduzi wa miradi ya maendeleo. Nitoe rai kwa wananchi wote kushiriki katika maadhimisho hayo yatakayofanyika tarehe 26 Aprili ili kuendelea kuenzi Muungano wetu.”
Mheshimiewa Majaliwa alisema Serikali imeendelea kuratibu vikao vya kamati ya pamoja kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ajili ya kushughulikia masuala ya Muungano.
Alisema katika mwaka 2025/2026 Serikali itahakikisha kwamba hoja za Muungano zilizopo na zitakazojitokeza zitashughulikiwa kikamilifu. Vilevile, itaendelea kutekeleza miradi na programu mbalimbali za maendeleo kwa lengo la kuudumisha na kuulinda Muungano huo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema nchi imeendelea kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 128, utoshelevu huo unatokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya chakula kutoka tani milioni 20.4 katika msimu wa kilimo wa 2022/2023 hadi tani milioni 22.8 msimu wa mwaka 2023/2024.
Pia, Waziri Mkuu amesema ongezeko hilo limetokana na ongezeko la matumizi ya mbolea iliyotolewa kwa wakulima kupitia mpango wa ruzuku, kuongezeka kwa mtandao wa kilimo cha umwagiliaji, kuimarika kwa huduma za ugani na matumizi ya mbegu bora.
