Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango, leo tarehe 24 Aprili 2025 ameondoka nchini kuelekea Vatican kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwenye Mazishi ya aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani hayati Baba Mtakatifu Francisko.
Misa ya Mazishi ya Papa Francisko inatarajiwa kufanyika tarehe 26 Aprili 2025, mbele ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro - Vatican na baadaye kufuatiwa na maziko yatakayofanyika katika Basilika ya Bikira Maria Majore (Santa Maria Maggiore).
