-Ataka itumike vizuri kujadiliana, kujenga hoja ili kuleta maelewano
-Ataka isitumika kuchochea shari kama wanavyofikiri baadhi ya wanasiasa
Na Mwandishi Wetu, Kongwa
Makamu wenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara Stephen Wasira, amesema maana ya demokrasia ni majadiliano, hoja na maelewano kwa lengo la kuimarisha umoja na ushirikiano katika kujenga taifa.
Amesema demokrasia sio vurugu kama ambavyo baadhi ya wanasiasa hususan wa vyama vya upinzani wanavyofikiri na kupiga kelele kutaka shari jambo ambalo CCM haikubaliani nalo.
Wasira alieleza hayo wilayani Kongwa Mkoa wa Dodoma akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025 ikiwa sehemu ya shughuli za kuelekea maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Tanzania ambao uliingiwa Aprili 26, mwaka 1964.
"Kama una hoja za kuwashawishi wapigakura wakukubali toa, kama huna kubali....kwa sababu hawana watu, uchaguzi wa serikali za mitaa wameshindwa kwa sababu hawana wagombea, sasa wanalalamika tumeibiwa mumeibiwa wapi?
"Vijijini humo hawana watu, hata mkienda kwenye kijiji cha Kongwa mkasema niitieni hata watu 10 wa CHADEMA nitakulipa, mtu atapata tabu sana na atakosa hela maana hawapo.


