Na. Hamis Dambaya
Uwepo wa taarifa za wanyama wakubwa watano maarufu duniani "Big 5" umevutia wanafunzi na walimu wa Vyuo vya Japan waliotembelea banda la Tanzania kwenye maonesho ya Osaka Expo 2025 yanayoendelea nchini Japan.
Wanyama hao ambao ni Simba, Tembo, Nyati, Faru na Chui wanaopatikana katika hifadhi ya Ngorongoro na hifadhi nyingine nchini Tanzania wamewafanya watembeleaji wa banda hilo hasa wanafunzi, wazazi na walimu kutumia muda mwingi kudadisi na kupata maelezo ya kina huku wakitamani kufika Tanzania kuwaona .
Baadhi ya walimu na wanafunzi wameeleza kuwa wameridhishwa na taarifa na elimu ya kutosha waliyoipata kuhusu namna wanyama hao wanavyoishi pamoja na tabia zao jambo ambalo linatoa msukumo kwao kufikiria namna wanavyoweza kuanza mipango ya kufanya utalii wa safari kwa Tanzania.
"Habari hizi ni Njema na hatujawahi kujuwa kuwa katika hifadhi wengi mtawanyiko wa Wanyama unahusisha uwepo wa Big 5 ambayo mtu anaweza kuiona ndani ya mda mfupi, tumesikia habari nyingi kuhusu uwepo wa vivutio vingi vya Utalii Tanzania vivutio vya kihistoria na Malikale zenye historia nyingi pamoja na bichi nzuri, tunaamini tutajipanga na kuja siku moja" alieleza Dkt. Takumi Keisuke kutoka Chuo kikuu cha Jiji la Osaka.
Akizungumzia hali hiyo Afisa Uhifadhi mkuu Masoko wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Michael Makombe amesema ari hiyo ya wajapan kutaka kufahamu mengi kuhusu wanyama hao hasa kwa watoto, vijana na taasisi za elimu imeongeza mwanga wa kuwaelimisha kuhusu suala zima la utalii wa wanyama ambao ni nadra nchini Japan.
Dr Gladstone Mlay kutoka Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA) amesema uamuzi wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Bodi ya Utalii Tanzania wa kuhamasisha utalii nchini Japan ni mwanzo mzuri katika utoaji wa elimu hasa kwa vijana ambao ndiyo watalii wa miaka ijayo.
Akizungumzia kuhusu fursa zilizopo nchini Tanzania hasa katika masuala ua uwekezaji na uwindaji Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa uhifadhi Lillian Wawa amesema kupitia EXPO 2025 Tanzania imeweza kuonesha fursa zilizopo katika uwekezaji wa sekta hiyo kwenye maeneo mengi yanayosimamiwa na Mamlaka zilizopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Wiki ya Utalii inaendelea nchini Japan ambapo Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Bodi ya Utalii nchini Tanzania inaendelea kuratibu mikutano na wadau mbalimbali pamoja na kutoa fursa kwa maafisa wanaoshiriki maonesho haya kukutana na watembeleaji na kuwapa elimu kuhusu fursa za utalii na uwekezaji zilizopo nchini.