Na. Anangisye Mwateba-Dodoma
Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) imeanzisha kampuni tanzu ya “Misitu Company Ltd”, ambayo pamoja na mambo mengine itajikita katika uendeshaji wa baadhi ya viwanda na biashara ya mazao ya nyuki.
Kampuni hiyo itakapokamilisha taratibu za uendeshaji itakuwa tayari kununua mazao ya nyuki kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwemo wananchi watakaohudumiwa na Kiwanda cha Asali cha Sao Hill.
Haya yamebainishwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula(Mb) alipokuwa akijibu swali la Mhe. Ritta Enespher Kabati ambaye alitaka kujua Kiwanda cha Asali cha Sao Hill kilichopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kitanunua Asali kutoka kwa Wananchi?
Mhe. Kitandula alisema Kiwanda cha kuchakata asali cha Sao Hill kwa kuanzia kinatoa huduma za uchakataji wa mazao ya nyuki yanayozalishwa na TFS pamoja na wananchi kutoka vijiji jirani.
Hata hivyo, kwa sasa kiwanda hakijaanza kununua mazao ya nyuki ikiwemo asali kutoka kwa wananchi kwa kuwa mfumo wa uendeshaji wa Wakala za Serikali hautoi mwanya huo kibishara’ Mhe. Kitandula.