Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga ameoneshwa kuridhishwa na kazi ya uimarishaji mpaka wa kimataifa kati ya Tanzania na Kenya.
"Nimefurahi na kuridhishwa kwa kazi iliyofanyika ya kuimarisha mpaka wetu na nduguzetu wa kenya na niseme ni mfano mzuri wa kazi ya uimarishaji mpaka kwa nchi tunazopakana nazo" amesema.
Mhandisi Sanga ameridhishwa na kazi hiyo alipotembelea kijiji cha Usongo na Horiri Mjini wilayani Rombo mkoa wa Kilimanjaro tarehe 23 Juni 2025 kuangalia maendeleo ya zoezi la uimarishaji mpaka wa kimataifa kati ya Tanzania na Kenya.
Kwa mujibu wa katibu mkuu wa wizara ya Ardhi, kati ya kilomita 758 za mpaka wa kimataifa kati ya nchi hiźo mbili tayari kilomita 558 zimeimarishwa na kueleza kuwa hilo ni jambo zuri na la kujipongeza.
Kwa upande wake Mratibu wa zoezi la uimarishaji mpaka wa kimataifa kati ya Tanzania na Kenya Bw. Robert Paul ameeleza kuwa, katika awamu ya nne na tano ya uimarishaji mpaka wa nchi hizo,Tanzania imetekeleza kazi zake zote kwa wastani wa asilimia 95.
Mpaka wa Tanzania na Kenya upande wa eneo la nchi kavu una ukubwa wa Kilomita 758 na uimarishaji wake mbali na mambo mengine utasaidia kuondoa baadhi ya changamoto zilizokuwa zikijotokeza kwa wananchi wanaofanya shughuli katika maeneo ya mipakani.