Polisi kata wa Mkoa wa Songwe wamepongezwa kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuyafikia makundi mbalimbali na kutoa elimu juu ya madhara ya imani za kishirikina, ulevi ulikithili, vipigo vilivyopitiliza, mimba za utotoni, ubakaji, uhalifu ikiwa ni pamoja na matendo yote maovu na kuendelea kufanya Mkoa wa Songwe kuendelea kuwa salama na jamii kuendelea kuliamini Jeshi la Polisi kwa kuleta taarifa fiche za uhalifu na wahalifu ili ziweze kushughulikiwa kwa haraka.
Pongezi hizo zimetolewa Juni 20, 2025 katika ukumbi wa Polisi Vwawa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Augustino Senga na kuwataka kuendelea kutoa elimu juu ya madhara ya uhalifu katika jamii kwa lengo la kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu katika jamii.
Aidha, Kamanda Senga amewataka Polisi Kata wote kuhakikisha wanashirikiana na watendaji wengine katika Kata husika kwa lengo la kuendelea kujenga ushirikiano ambao utapunguza uhalifu katika maeneo yao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Operesheni Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Nicholas Livingstone amewataka Polisi kata hao kuendelea kutoa huduma bora kwa jamii ikiwa ni pamoja na kutoa elimu juu ya zoezi la uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi wa kumi mwaka 2025.