“Tuna waumiza watoto”
Katika mila na tamaduni nyingi za Kiafrika, mshikamano wa kifamilia ni msingi wa maisha. Kuishi na kusaidiana kama ndugu limekuwa jambo la kawaida, lenye kuonekana kama ishara ya utu, upendo na mshikamano. Familia nyingi zimewafungulia milango ndugu waliopoteza kazi, waliotalikiana, waliotoka vijijini au waliokumbwa na changamoto mbalimbali. Kwa moyo mweupe, wamepewa hifadhi, chakula, na nafasi katika familia hizo.
Lakini leo, kuna ongezeko kubwa la simulizi za maumivu. Watu waliokaribishwa kama ndugu wamegeuka kuwa chanzo cha huzuni, mateso, na hata maangamizi ya familia.
Maisha ya kumsitiri ndugu – Ndoto iliyogeuka kabusu
Katika jamii zetu, kumkaribisha ndugu nyumbani ni jambo la kawaida. Lakini hali imebadilika sana. Baadhi ya ndugu wamekuwa wakiharibu maisha ya watoto wa familia nyingi kwa ukaribu waliokuwa nao na kutumia kigezo cha imani ya undugu kwa kuwadhulumu kimwili na kihisia. Mjomba, baba wadogo, na hata kaka wa kambo wamegeuka kuwa wakosaji wa maadili na hata kukosa hofu ya Mungu kwa kutumia nafasi waliyopewa kuharibu watoto, kwa kuwaingila kimwili kwa ulazima wakiwa na umri mdogo na hata wengine kuwafanyia majaribio ya kingono na wengine huenda mbali zaidi kwa kuwaingilia watoto kinyume na maumbile. Huku wakiwapa maneno ya vitisho na kuwalaghai kwa vitu vidogo vidogo. Hivyo kupelekea watoto hao kujenga uoga kwa kuangalia kigezo cha ukaribu na imani ya undugu uliopo lakini pia hofu ya mapokeo ya wazazi endapo mtoto huyo ataamua kusema ukweli. Hivyo kupelekea watoto hao kupambana kimya kimya na wengine kuendelea kuishi katika mazingira ya unyanyasaji pasipo na mahali pakusemea na mzazi kutokujua kinacho endelea.
Lakini tumeshuhudia mara nyingi wapo wanawake waliopoteza ndoa zao kwa sababu dada au binamu aliemkaribisha nyumbani kwa upendo alianzisha mahusiano ya siri na mume wake, na hata kubeba mimba za shemeji zao na kupelekea mpaka ndoa kuvunjika.
Watoto Wanaumia Kimya Kimya:Ukimya wa uchungu kulinda undugu
Watoto wengi wanaoishi kwenye familia zenye ndugu wa kuokota wamekuwa waathirika wakubwa wa unyanyasaji wa kingono. Mtoto anapofanyiwa kitendo cha unyanyasaji na mjomba au baba mdogo, anabaki na maswali mengi yasiyo na majibu. Anasikia aibu, anaumia, na mara nyingine anajilaumu mwenyewe na kuamua kunyamaza kwa hofu. Na ni ukweli usio pingika wengi wao hawawezi kusema kwa sababu wanaogopa:
Kutoaminika na wazazi wao.....
Kutishiwa na wanaowatendea hayo mambo
Kuharibu mahusiano ya kifamilia (undugu)
Hapo ndipo mzazi anapopaswa kujiuliza: Je, mtoto wangu ana mahali salama pa kusema?
Mzizi wa uharibifu wa watoto wa kiume: safari ya maumivu inayoanzia nyumbani
Katika simulizi nyingi za vijana wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja (hasa wa kiume), chanzo chake kimekuwa ni unyanyasaji wa kingono wa utotoni – wakitendewa mabaya na ndugu wa familia. Kwa sababu hakuna aliyejua, hakuna aliyewasaidia na hakuna lie yaona maumivu yao ya kimya kimya, walibeba maumivu hayo hadi ukubwani, na hivyo kuishia kwenye maisha ya kuchanganyikiwa, fedheha, na kuumia zaidi na huo ndio ukweli mchungu kuwa tatizo halianzi mtaani – linaanzia nyumbani na wakati mwingine, mchawi si jirani – ni yule ndugu tuliyempa kitanda sebuleni au chakula mezani, ulie muamini na kumpatia nafasi ya kuwa na ukaribu na watoto wako kwa nafasi yoyote ile aliyo ihitaji kwa wakati wake ili kuweza kuyatimia maovu yake. Huku wazazi wakibaki kuilaumu mitandao na mifumo ya elimu mashuleni pasipokujua wanao haribu na kuwaumiza watoto wetu tumewakumbatia manyumbani kwetu.
Wazazi, tujitafakari: tunawajua watoto wetu kwa kina?
Maisha ya utafutaji kutoka usiku na kurudi usiku yameleta changamoto kubwa sana kwenye suala la malezi na kupelekea wazazi wengi kuto kuwajua watoto kwa kina na hata wakati mwingine kushindwa kuzisoma hisia za mtoto kimya kimya kwa kuangalia mienendo yake na mabadiliko ya tabia zake ili kubaini yale yaliyo jificha. Na hili ni jukumu kubwa kwa mazazi kuhakikisha anakuwa na uwezo wa kisaikolojia wa kuzisoma hisia za mtoto kulingana na mabadiliko madogo madogo ya tabia zake ili kubaini kinacho msumbua.
Lakini pia ukali wa kupitiliza kutoka kwa wazazi unawanyima watoto nafasi ya kusema yale wanayo kumbana nayo , ni muhimu wazazi kuachana na dhana ya kulea watoto kizamani na kujitahidi kujenga mahusiano ya karibu na ya wazi na watoto wao, mahusiano yenye uhuru wa kuzungumza , kujielezea na kushirikiana kihisia. Wazazi tujenge tabia ya kusikiliza zaidi kuliko kutoa hukumu kwa watoto.Maumivu ya watoto hawa yanaweza kuzuilika kama wazazi wataacha kuwa “watu wa milipuko” na kuwa “walinzi wa kweli”.
Tuamke Kama Jamii
Ni wazi kuwa maumivu mengi ya watoto wetu yamekuwa yakifichwa nyuma ya ukuta wa heshima kwa ndugu, hofu ya jamii, na ukimya unaoua. Sasa ni wakati wa kusema imetosha.
1. Wazazi Tujenge Mahusiano ya Kuaminiana na Watoto:
Watoto wasikie kuwa na uhuru wa kusema lolote bila kuhukumiwa. Uliza maswali, zungumza nao kwa upendo, sikiliza hisia zao kila siku.
2. Kujenga Uelewa kwa Familia na Jamii:
Fanya mazungumzo ya wazi kuhusu mipaka ya maadili ndani ya nyumba. Jamii iache tabia ya kuficha maovu kwa jina la “kulinda heshima ya familia.”
3. Kufundisha Watoto Kutambua na Kuripoti Unyanyasaji:
Wape elimu ya miili yao, wape ruhusa ya kusema "hapana", na wafundishe kwa lugha wanayoelewa kwamba kuna mambo wasikubali kufanyiwa hata na mtu wa familia.
4. Kutoa Elimu Kwenye Makanisa, Misikiti, na Shule:
Viongozi wa dini na walimu wa shule washirikishwe kuwa sehemu ya kampeni dhidi ya ukatili wa kindugu na sio wa majiranik au watu wasio julikana peke yake, kwa kutoa mafundisho ya maadili na ulinzi wa watoto.
5. Kuweka Mipaka ya Kuishi na Ndugu:
Wazazi wasiwe wepesi kuingiza watu wa ukoo ndani ya nyumba bila tathmini ya tabia na madhara yake kwa watoto. Sio kila ndugu anafaa kuwa mlezi.
6. Sheria Kuchukua Nafasi Yake:
Wazazi na walezi wasisite kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama pindi wanapobaini mtoto amefanyiwa unyanyasaji na ndugu wakaribu. Kuficha ni kushiriki kosa.
Hitimisho:
Ni lazima tukubali kuwa si kila ndugu anafaa kuingizwa kwenye mfumo wa familia zetu. Moyo wa huruma usiwe kipofu. Tunaishi kwenye nyakati ambapo watu wamekosa utu, hofu ya Mungu imepungua, na tamaa imejaa. Ukarimu wetu usigeuke kuwa shimo la maangamizi kwa watoto na familia zetu. Jamii yetu ipo hatarini. Tunawapokea ndugu kwa moyo mmoja, lakini wengine wanarudisha shukrani za majeraha. Tunapowakaribisha ndugu, tusiache hekima nyuma. Tujifunze kusema “hapana” pale inapobidi na kuweka mipaka juu ya dhana ya kusaidiana ili kuokoa ndoa zetu na watoto wetu.
Tuamke, Tuchukue Hatua.
Je, una maoni au simulizi kama hili?Tafadhali shiriki nasi kupitia sehemu ya maoni hapa chini. Saidia kuelimisha wengine kwa kusambaza makala hii. Kumbuka – mabadiliko huanza na sisi.
Imeandikwa na Na. Sharon Chamwingi Mpondachuma