Wanafunzi zaidi ya kumi kutoka Doha, nchini Qatar, wakiambatana na walimu na baadhi ya wazazi wao, wametembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini Tanzania ikiwa ni sehemu ya kujifunza na kujionea utajiri wa maliasili uliopo nchini.
Katika ziara hiyo iliyopewa jina la “Thedi Kilimanjaro Expedition”, wanafunzi hao walipata fursa ya kupanda Mlima Kilimanjaro, kutembelea maporomoko ya maji, pamoja na hifadhi mbalimbali za wanyamapori. Wameeleza kuvutiwa na mandhari ya kuvutia ya Tanzania na kuahidi kuwa mabalozi wazuri wa kuitangaza nchi hiyo kama kivutio cha utalii pindi watakaporejea nchini kwao.
Ziara hiyo imeratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Tanzania, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali kutangaza utalii wa Tanzania katika soko la kimataifa, hususan nchini Qatar, ambayo ina nafasi kubwa ya kukuza sekta hiyo kupitia usafiri wa kimataifa.
Godwin Kiegeko, Afisa wa Mambo ya Nje kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, amesema ujio wa wanafunzi hao utakuwa kichocheo cha wageni wengine wengi kuitembelea Tanzania, hasa vijana kutoka mataifa ya Kiarabu.
Kwa upande wake, Afisa Utalii Mkuu kutoka Bodi ya Utalii Tanzania, Ester Solomoni, amesema kuwa kupitia ziara hiyo, soko la utalii wa Tanzania nchini Qatar litazidi kukua, na hivyo kusaidia kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania kila mwaka.
Abrahamani Saidi, mmoja wa wakufunzi waliowasindikiza wanafunzi hao, amesema kupanda Mlima Kilimanjaro ilikuwa ni fursa ya kipekee kwa wanafunzi wao. Wamejifunza kuhusu jiografia, ikolojia na pia umuhimu wa uhifadhi wa mazingira. Pia wameweza kuona utofauti mkubwa wa kijiografia na tamaduni baina ya Tanzania na Qatar.
Nao wanafunzi kutoka nchi hiyo wakaelezea mazingira na waliyojifunza na kujivunia walipotembelea Mlima Kilimanjaro:
• Abdalla Mufta, mwanafunzi kutoka Qatar
• Dima, mwanafunzi kutoka Qatar
• Yusuph Sahala, mwanafunzi kutoka Qatar
Ziara hiyo imeacha alama kubwa kwa washiriki na kuonyesha nafasi ya Tanzania kama kituo muhimu cha utalii wa kielimu na kiutamaduni katika ukanda wa Afrika Mashariki.