-Mhandisi Luoga asema mafunzo hayo ni endelevu kwa Watendaji na Wataalam katika Sekta ya Nishati
Watendaji kutoka Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati wamepata mafunzo kuhusu Ufuatiliaji na Tathmini ambayo yanalenga kuziwezesha Taasisi hizo kuendelea kuboresha utendaji kazi.
Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga amefunga mafunzo hayo leo jijini Dodoma kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba ambapo amewataka watendaji hao kutumia ujuzi walioupata kuboresha utendaji kazi, uwajibikaji na utekelezaji wa miradi iliyopo chini ya Wizara.
“Mafunzo mliyoyapata ya ufuatiliaji na tathmini yawe kichocheo cha kimkakati katika utendaji kazi, uwajibikaji na uboreshaji endelevu wa utekelezaji wa miradi mbalimbali iliyopo chini ya Wizara ya Nishati." Amesema Mha. Luoga.
Amesema Wizara itaendelea kuwajengea uwezo watendaji na wataalam waliopo katika Sekta ya Nishati nchini kwa kutoa mafunzo ambayo yataendelea kuboresha utendaji kazi.
Mha. Luoga amekipongeza Chuo Kikuu cha Mzumbe ambacho kimetoa mafunzo ya Ufuatiliaji na Tathmini kwa watendaji hao wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati.
Taasisi za Wizara ya Nishati zilizohudhuria mafunzo hayo ni Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO), Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli ( PURA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania ( TPDC), Wakala wa Nishati Vijijini ( REA) na Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA).