Pembeni ya Ufukwe wa Ziwa Tanganyika, katika safu za Milima ya Mahale iliyoko wilayani Uvinza, mkoani Kigoma, ndiko linapopatikana eneo la kipekee linalohifadhi mnyama aina ya sokwe. Sokwe huyu anayefanana na binadamu kwa asilimia 98.6, anapatikana kwa wingi katika Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Mahale, ambapo inakadiriwa kuwa asilimia 93 ya sokwe wote waliopo nchini wanaishi katika hifadhi hiyo.
Licha ya umbali kutoka Kigoma mjini, Hifadhi ya Taifa ya Mlima ya Mahale imeendelea kuvutia wageni wengi, ambapo mwaka 2023/24 iliwakaribisha watalii 923. Idadi hii inaelezwa kuwa matokeo ya juhudi kubwa za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia kampeni yake ya 'Royal Tour', ambayo imetangaza vivutio vya utalii nchini, ikiwemo Mahale kama "nyumbani kwa sokwe."
Kutokana na upekee huo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula, alifanya ziara katika Hifadhi ya Mahale ili kujionea hali halisi ya hifadhi hiyo ambayo bado haijaguswa na shughuli za kibinadamu, tofauti na hifadhi nyingi nchini. Alisema kuwa hifadhi hiyo ni miongoni mwa maeneo bora duniani kwa utulivu na mvuto wa kipekee wa kiasili.
Mhe. Kitandula alibainisha kuwa sekta ya maliasili na utalii ni miongoni mwa maeneo yaliyopewa kipaumbele katika Dira ya Taifa 2025–2050, kwa kuwa inatarajiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa pato la taifa. Aliwataka wahifadhi kutumia fursa hiyo kuongeza juhudi ili kuishawishi serikali kuwekeza zaidi katika uhifadhi na maendeleo ya utalii.
Akizungumzia maendeleo ya miundombinu, Mhe. Kitandula alisema kuwa ujio wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Musongati nchini Burundi hadi Uvinza ni fursa kwa Hifadhi ya Mahale kuvutia watalii zaidi kutoka ukanda wa Mwanza na Burundi.
Katika ziara hiyo, Mhe. Kitandula alipata fursa ya kuzungumza na maofisa na askari wa hifadhi, akiwapongeza kwa kazi kubwa ya uhifadhi na kuwaahidi kuwa serikali itaendelea kuboresha mazingira yao ya kazi, ikiwemo kuwapatia vitendea kazi na kuboresha maslahi yao.
Aidha, alitembelea pia baadhi ya kambi za watalii zilizopo ndani ya hifadhi, ikiwemo Kasia Bandas, Nomad Greystoke Mahale, na Mbalimbali Camp & Lodge, ili kujionea uwekezaji uliofanyika na kutathmini mchango wake katika kukuza utalii katika eneo hilo.











