-Miundombinu ya Michezo Zanzibar Yavuka Kiwango cha Kimataifa kuelekea CHAN
Zanzibar, Julai 22, 2025
Serikali imeridhishwa na maandalizi ya miundombinu ya michezo Zanzibar kuelekea Mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), huku Uwanja wa Amaan Complex ukitajwa kuwa katika viwango vya kimataifa.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim Yonazi, mara baada ya kuongoza Kamati ya Makatibu Wakuu kukagua maandalizi ya CHAN katika visiwa vya Zanzibar.
“Tumejionea hali halisi ya miundombinu, hasa Uwanja wa Amaan. Uko katika viwango vya kimataifa, na tunaamini Zanzibar ipo tayari kuwa sehemu ya mashindano haya muhimu kwa bara letu la Afrika,” amesema Dkt. Yonazi.
Aidha, Dkt. Yonazi alieleza kuwa hatua hiyo inaonesha utayari wa Taifa kuandaa mashindano ya kimataifa, huku akisisitiza kuwa mashindano ya CHAN ni fursa kubwa ya kuimarisha michezo na kukuza uchumi wa ndani.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo (SMZ), Mhe. Fatma Hamad Rajab, alieleza kuwa Uwanja wa Amaan Complex tayari umekidhi vigezo vyote vinavyohitajika na Zanzibar iko tayari kuwapokea wachezaji, mashabiki na wageni kutoka mataifa mbalimbali.
Kamati hiyo ya Makatibu Wakuu inafanya ziara katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani ili kukagua maandalizi ya CHAN na AFCON 2027.
Mashindano ya CHAN yanatarajiwa kuanza rasmi tarehe 2 Agosti 2025 yakihusisha wachezaji wanaocheza ligi za ndani kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika.