![]() |
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imedhamiria kufanya kampeni kubwa za kuhamasisha utalii wa ndani kwa kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kuendelea kuongeza idadi kubwa ya watanzania kutembelea hifadhi ya Ngorongoro.
Akizungumza katika maonesho ya biashara ya kimataifa jijini Dar es Salaam Kamishna Msaidizi Mwandamizi huduma za utalii na masoko Mariam Kobelo amesema kampeni hizo zitajikita katika maeneo ya shule, vyuo na taasisi za umma na binafsi.
“Kati ya Julai 2024 hadi Juni 2025 Watalii waliotembelea Ngorongoro walikuwa 419,166, tumeamua kuongeza nguvu katika kutangaza utalii wa ndani ili kuwawezesha watanzania wengi zaidi kufahamu vivutio ambavyo hifadhi hiyo inavisimamia,”alisema Kamishna Msaidizi Mwandamizi Mariam.
Ameeleza kuwa hifadhi hiyo ina vivutio vingi ikiwemo kreta ya Ngorongoro yenye wanyama wa aina zote, bonde la Olduvai Gorge, tambarare za Ndutu, mchanga unaohama, Nyayo za Laetoli mapango ya Amboni na Kimondo.
Takwimu zinaonesha kuwa idadi ya watalii wa ndani imekuwa ikiongezeka na mwaka wa fedha 2024/2025 idadi ya watalii wa ndani ilikuwa 419,166 ambapo mpango wa NCAA ni kuongeza zaidi kupitia kampeni mbalimbali za Utalii wa Ndani kwa watanzania.
![]() |