Kutokana na ongezeko la shule za udereva nchini kote zenye lengo la kuwapatia vijana maarifa sahihi ya kuendesha magari kwa usalama na kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani Jeshi la Polisi limebainisha changamoto kadhaa hasa katika matumizi ya magari chakavu pamoja na walimu wasiokuwa na ujuzi wa kutosha kwa kuwajengea uelewa wanafunzi wanaotaka kuwa madereva.
Hayo yamesemwa Julai 16, 2025 na Mkuu wa Usalama Barabarani Nchini, (DCP) Freser Kashai alipofanya ukaguzi katika Shule ya Udereva Mbozi iliyopo Kata ya Ichenjenzya Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe na kuwataka wamiliki wa shule za udereva kutumia magari yenye hali nzuri katika mafunzo ya udereva yenye mifumo ya usalama kama breki, taa, honi na mikanda ya viti inayofanya kazi ipasavyo kwani magari chakavu huongeza hatari ya ajali kwa wanafunzi ambao bado wanaanza kujifunza mbinu za uendeshaji ili waje kuwa madereva bora wanaofuata sheria za usalama barabarani.
"Mnatakiwa mtumie magari mazima ikiwa ni ishara ya uwajibikaji wa shule za udereva kwa wanafunzi na kwa jamii kwa ujumla ikiwa ni pamoja na walimu wa udereva wanapaswa kuwa na leseni halali ya kufundisha na uzoefu wa kutosha katika kuendesha na kufundisha kwa njia bora ili kutengeneza madereva wenye uelewa wa kufuata sheria za usalama barabarani ambao watakuwa siyo chanzo cha ajali" alisema DCP Kashai.
"Walimu wenye ujuzi husaidia wanafunzi kuelewa kwa kina sheria za usalama barabarani kujua mbinu salama za uendeshaji na kufanya maamuzi sahihi katika mazingira hatarishi ili kuepusha au kujiepusha na ajali zinazoweza kuepukika" alisisitiza DCP Kashai.
Aidha, DCP Kashai alisema kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kuhakikisha shule za udereva zimesajiliwa na zinafuata viwango vilivyowekwa ikiwa ni pamoja na kufanyiwa ukaguzi wa mara kwa mara wa vifaa vya shule na uwezo wa walimu kwani utasaidia kuinua ubora wa mafunzo ya udereva na kupunguza ajali barabarani.
Pamoja na hayo, DCP Kashai aliwaeleza kuwa shule za udereva zina mchango wa mkubwa katika kuandaa madereva wa kesho, ili kuhakikisha usalama na ufanisi ni lazima zitumie magari mazima na kuwa na walimu wenye sifa stahiki kwa ustawi wa madereva bora ambao watapunguza ajali za barabarani.