TANGAZO

TANGAZO

UREJESHAJI MIKOPO REKODI YAVUNJWA 2024/2025



Na. Mwandishi wetu, Dar es salaam

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imevunja rekodi ya ukusanyaji wa mikopo iliyoiva kwa kufanikisha kukusanya TZS 194.5 bilioni katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025, kiasi ambacho hakijawahi kufikiwa miaka ya nyuma.

Akizungumza na watumishi wote wa HESLB katika kikao cha kufunga mwaka 2024/2025 kilichofanyika hivi karibuni katika ofisi za HESLB zilizopo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia alisema kuwa kiwango hicho cha ukusanyaji ni 97% ya lengo lililokuwa limewekwa la kukusanya TZS 199 bilioni.

Pamoja na pongezi kwa menejimenti na watumishi kuwezesha kukusanya kiasi hicho cha fedha za mikopo iliyoiva, Dkt. Kiwia aliwataka watumishi kuongeza jitihada ili kuhakikisha mwaka huu mpya 2025/2026 wanaendelea kufanya vizuri katika makusanyo.

“Tuna kibarua cha kukusanya TZS 210 bilioni mwaka 2025/2026 … muongeze jitihada kwani tumeendelea kuaminiwa na serikali … tuzidi kuboresha utendaji kazi na kupeana moyo ili kufikia malengo”, alisema Dkt. Kiwia.

Akizungumza baada ya mkutano na kupokea pongezi kutoka kwa watumishi, Mkurugenzi wa Urejeshaji na Urejeshwaji Mikopo Bw. George Mziray alieleza kuwa mafanikio waliyoyafikia katika ukusanyaji mikopo yametokana na mikakati iliyowekwa inayosimamiwa na Menejimenti kwa ujumla chini ya Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Bill Kiwia.

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, makusanyo ya mikopo kutoka kwa wanufaika ambao mikopo yao imeiva yamekuwa yakipanda kwa kiasi cha kuridhisha ambapo mwaka 2023/2024 zilikusanywa TZS 177 bilioni na mwaka uliotangulia wa 2022/2023 zilikusanywa TZS 169 bilioni.




Kama una Taarifa,Picha, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kwa simu +255 766 166 125 au Email : emmymwaipopo@gmail.com