Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula, amesema kuzinduliwa kwa makumbusho maalum ya kuhifadhi na kuenzi urithi wa kitaaluma, kitamaduni na kihistoria wa taifa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ni alama isiyofutika katika historia ya elimu na maendeleo ya jamii nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo chuoni hapo leo, Mhe.Kitandula amesema makumbusho hayo yatatoa fursa kwa wanafunzi, watafiti na wadau mbalimbali kuunganishwa na urithi wa kielimu wa UDSM na taifa kwa ujumla.
“Makumbusho haya yanafungua ukurasa mpya wa historia kwa kuhakikisha urithi huu unahifadhiwa, kuenziwa na kuhamasisha vizazi vijavyo kufanikisha malengo makubwa zaidi,” amesema.
Aidha, amebainisha kuwa wizara yake itaendelea kushirikiana na UDSM kuhakikisha makumbusho hayo yanakuwa kivutio cha utalii wa kiutamaduni na kielimu kwa watalii wa ndani na wa kimataifa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, Balozi Mwanaidi Sinare Maajar, amesema makumbusho hayo yatakuwa jukwaa la kuunganisha wataalamu wa uhifadhi kutoka ndani na nje ya nchi.
Awali, Makamu Mkuu wa UDSM, Prof. William Anangisye, amesema makumbusho hayo yatatumika kama darasa hai kwa vizazi vya sasa na vijavyo na yatachochea uelewa mpana kuhusu historia ya kitaaluma na utamaduni wa taifa.





