TANGAZO

TANGAZO

OFISI YA MAKAMU WA RAIS YAANZA KUTEKELEZA AGIZO LA RAIS SAMIA



Ofisi ya Makamu wa Rais imeanza kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu suala la Uhifadhi na Utunzaji wa Mazingira katika Mradi wa Mto Mkuju wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma.


Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja akiwa katika ziara mkoani humo amesema, Rais Dkt. Samia alitoa maelekezo hayo Juni 30, 2025 wakati akifungua kiwanda cha Majaribio cha Kuchenjua Urani katika eneo la mto Mkuju wilayani humo.

“Ziara hii ni maelekezo ya Mhe. Rais aliyoyatoa wakati anazindua kiwanda hiki, kwamba Ofisi ya Makamu wa Rais ifike mara moja na kuangalia namna gani kiwanda kimechukua hatua kwenye masuala ya mazingira sababu ni kiwanda ambacho kinazalisha urani hivyo lazima tuhakikishe uzalishaji wa madini ya urani katika mradi usije ukaathiri mazingira.

“Tumekuja na kujilidhisha lakini pia na kujifunza sababu ni jambo jipya na ni kiwanda kipya hapa nchini cha urani hivyo tunatakiwa kuangalia namna gani mazingira yanatunzwa ipasavyo,” amesema Luhemeja.

Ameongeza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alielekeza kuwa baada ya kukagua mradi huu wa madini ya urani, wanapaswa kwenda nchini Namibia kujifunza na kuangalia namna ambavyo wao wanavyofanya katika eneo la Urani.

Amesema wameangalia na kugundua namna ambavyo mwekezaji amejitahidi kuhakikisha mazingira yatakuwa salama katika kiwanda hicho kwa kuweka mifumo ya usimamizi wa mazingira , kuwa na wataalam pamoja na kufuata taratibu zinazotakiwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma Mhe. Ngollo Malenya amesema mradi huo ni fursa kubwa kwa wananchi wa wilaya hiyo kwani utawainua wengi kiuchumi.

“Ukiangalia kwenye pato la Taifa sasa hivi tutakuwa tunachangia kwa asilimia kubwa na mradi huu utakuwa chachu ya maendeleo na nitoe wito kwa wananchi kuwa tayari kuchangamkia fursa”.

Ameongeza kuwa mradi huo kufanyika katika wilaya hiyo ni faraja kubwa sio kwa wananchi wa Nmtumbo bali Tanzania nzima kwa kuwa itawagusa wengi katika eneo tofauti ikiwa pamoja na vijana kupata ajira.

Naye Meneja wa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Mhandisi Boniphace Guni amesema wawekezaji wamejitahidi kwa asilimia kubwa kuhakikisha mifumo ya mazingira imewekwa ipasavyo.

Hata hivyo Meneja Mradi Bw. Beria Vorster ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa namna ambavyo inatoa ushirikiano katika kuhakikisha wanafanikisha lengo la mradi huo kwa kushirikiana na wataalamu ambao wengine ni raia wa Tanzania.

“Tanajitahidi kuhakikisha tunafuata taratibu zote ambazo zinapaswa kuzifuata ikiwemo suala la utunzaji na uhifadhi wa mazingira hilo tumelipa kipaumbele katika mradi wetu ndio maana kuna wataalamu ambao wanasimamia mazingira,” amesema Bw. Vorster.





Kama una Taarifa,Picha, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kwa simu +255 766 166 125 au Email : emmymwaipopo@gmail.com