Chini ya Rais Samia, huduma za afya ya mama na mtoto zimeimarishwa na kuongezeka kwa upatikanaji wake.
Idadi ya akina mama waliojifungua katika vituo vya afya imeongezeka kutoka 52,585 mwaka 2020 hadi 141,386 mwaka 2024.
Vilevile, watoto wachanga waliozaliwa hai wameongezeka kutoka 1,392,634 mwaka 2020 hadi 1,828,285 mwaka 2024. Serikali pia imejenga vyumba maalumu 114 vya huduma za dharura kwa watoto wachanga (Neonatal Care Unit na Kangaroo Mother Care).
Neonatal Care Unit (NCU) hii ni wodi au chumba maalumu cha hospitali kinachotunza watoto wachanga waliozaliwa njiti (kabla ya muda), wenye uzito mdogo, au wanaohitaji uangalizi wa karibu kutokana na matatizo ya kiafya baada ya kuzaliwa. Hapa hupata vifaa na huduma za kitaalamu kama oksijeni, ufuatiliaji wa mapigo ya moyo, na lishe maalumu.
Aidha, Kangaroo Mother Care (KMC) hii ni mbinu ya kumtunza mtoto njiti au mwenye uzito mdogo kwa kumuweka kwenye kifua cha mama kwa mguso wa ngozi kwa ngozi (skin-to-skin contact). Mbinu hii husaidia kudhibiti joto la mwili wa mtoto, kuboresha kupumua, kuongeza ulishaji wa maziwa ya mama, na kuimarisha uhusiano kati ya mama na mtoto.
