Polisi Kata Mkoa wa Songwe wametakiwa kuhakikisha wanaendelea kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi katika maeneo yao kuhusu umuhimu wa kudumisha amani, utulivu na kuheshimu sheria.
Kauli hiyo imetolewa Agosti 07, 2025 na Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Maria Kway alipofanya kikao na Wakuu wa Polisi Jamii Wilaya na Polisi kata Mkoa wa Songwe katika ukumbi wa Polisi Vwawa Wilaya ya Mbozi Mkoani humo, na kusema kuwa uchaguzi ni haki ya kidemokrasia ya kila Mtanzania, na ni jukumu letu kama walinzi wa raia na mali zao kuhakikisha kuwa mchakato huu unafanyika kwa amani bila uvunjifu wa sheria.
”Fanyeni mikutano katika makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na viongozi wa Vitongoji,Vijiji, Mitaa, dini na vijana ili kujenga uelewa wa pamoja kuhusu umuhimu wa uchaguzi wa amani, pia toeni elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya uchochezi, lugha ya matusi, na vitendo vinavyoweza kusababisha vurugu ili uchaguzi ufanyike kwa amani na usalama” alisema ACP Kway.
ACP Kway, aliwataka Polisi kata hao kushirikiana na wadau mbalimbali katika jamii kutoa elimu kwa kwa wananchi kuhusu madhara ya uvunjifu wa amani katika uchaguzi na amewataka Polisi kata hao kuwataka wananchi katika maeneo yao kushiriki katika uchaguzi kwa amani, kuheshimu maamuzi ya wengine, na kuepuka vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa jamii.
Pamoja na Kikao hicho, Afisa Mnadhimu wa Polisi Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Akama Shaaban kwa upande wake, aliwasisitiza Polisi kata hao kusimamia sheria kwa haki na bila upendeleo na kuchukua hatua stahiki kwa yeyote atakayevunja sheria ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hizo.