Chama cha Wafanyakazi wa vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA), kimekabidhiwa rasmi cheti cha kutambulika kuwa mwanachama wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).
Aidha Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Tumaini Nyamhokya amewataka waandishi kujiunga na JOWUTA ili kuweza kudai haki zao na mambo mengine kwa pamoja.
Cheti hicho kimekabidhiwa leo Ijumaa Agosti 15,2025 jijini Arusha na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete kwa Mwenyekiti wa Jowuta, Musa Juma.
Makabidhiano hayo yalifanyika kwenye hafla ya uzinduzi wa jengo la biashara la Shirikisho hilo, lililopo jijini Arusha, ambapo Ridhiwani alikuwa mgeni rasmi
Akizungumza mara baada ya mabidhiano hayo, Rais wa TUCTA, Nyamhokya, amesema kujiunga kwa JOWUTA kunafanya Shirikisho hilo sasa kuwa na jumla ya vyama 16 kutoka 13 vilivyokuwa awali.
Kutokana na hatua hiyo, Nyamhokya aliwashauri waandishi kujiunga na chama hicho ili kuendelea kupata fursa mbalimbali zikiwemo kutetewa maslahi yao na elimu kuhusiana na masuala yanayohusu kazi.
Rais huyo amesema ukiacha Jowuta, Vyama vingine vipya vilivyopewa vyeti ni Chama cha Wafanyakazi sekta ya Ulinzi Binafsi (Tupse) na Chama cha Wafanyakazi wa Huduma za Viwandani Tanzania (Tasiwu).
Akizungumzia hatua hiyo,Mwenyekiti wa Jowuta, Musa Juma amesema, hatua hiyo ni ya muhimu kwao na kuahidi ushirikiano na TUCTA kupigania maslahi ya waandishi.
Kwa upande wake Waziri Ridhiwani, amesema TUCTA ina umuhimu na historia kubwa katika nchi hii kabla ,wakati na baada ya uhuru.
"Ambaye haoni kama shirikisho hilo lina umuhimu katika nchi hii, huyo hatakuwa mzalendo.
Pia hata mafanikio yote ambayo serikali inajivunia leo huwezi kuacha kuwataja wafanyakazi ikiwemo mafanikio katika sekta ya elimu, ujenzi wa SGR au mafanikio ya bandari, kwa hiyo muelewe hakuna siku serikali itawadharau na kuwasahau wafanyakazi,"amesema Ridhiwani.
Uzinduzi wa Jengo
Kuhusu jengo lililozinduliwa, Waziri huyo amesema imeonyesha namna vyama hivyo vimeamua kuunga mkono serikali katika uchumi na maendeleo ya kijamii kwa kuwa halitakuwa tu na faida kwa TUCTA bali kuchangia ukusanyaji kodi.
"Uwekezaji katika jengo hili unasaidia kataka kukuza ustawi wenu na utoaji huduma kwa jamii.
"Hivyo nitoe rai kwenu TUCTA kulitumia jengo hili katika kuendeleza mshikamano kwa kuwa kwa kufanya hivyo mtajenga taasisi iliyo imara na kuzidi kuaminiwa na serikali," alisema.
Awali akizungumzia mradi huo, Rais wa TUCTA amesema jengo hilo lilianza kujengwa miaka ya 1975 miaka ya 1990 jengo hili likamaliziwa kwa kuingia mkataba na wafanyabiashara kujenga vibanda.
Hata hivyo ujenzi wa awamu hii amesema umefanyika kuanzia mwaka 2023 likiwa limemalizika kwa asilimia 98 na kuna jumla ya wapangaji 138 ambao kwa mwezi wanaingiza zaidi ya shilingi milioni 50 kwenye shirikisho.
"Mbali na vyumba vya biashara pia jengo hili lina hoteli na chumba maalum (Presidental suit)," amesema Nyamhokya.



