Mgombea wa Urais kupitia tiketi ya chama cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuchanja mbunga kusaka kura za wananchi ambapo jana ameendelea kufanya ziara katika jimbo la Bahi katika mkoa wa Dodoma.
Katika hali inayoonyesha kukubalika kwake kwa wananchi mkutano huo ulihudhuriwa na mamia kwa maelfu ya watu licha ya mkutano huo kufanyika mapema asubuhi. Katika mkutano huo Dkt. Samia aliambatana na viongozi mbalimbali wa kitaifa akiwemo, Naibu Katibu mkuu ndg John Mongela, Katibu wa itikadi na Uenezi Ndg. Kenan Kihongosi, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dodoma Ndg. Adam Kimbisa na viongozi viongozi mbalimbali.
Kupitia mkutano huo Dkt. Samia alinadi sera zake sambamba na kuwanadi wagombea wa ubunge na Udiwani kupitia CCM.
ELIMU
Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa endapo serikali ya CCM itaendelea kuchaguliwa kwenye uchaguzi mkuu ujao, itaendelea kutoa elimu bila ada kwa wanafunzi wa wilaya ya Bahi, sambamba na kujenga Mabweni ya wanafunzi hasa shule za kike katika wilaya ya Bahi sambamba na kuendeleza miundombinu ya shule zote za jimbo la Bahi.
MAJI
Kuhusu sekta ya maji Dkt. Samia Suluhu Hassan ameahidi kumaliza kabisa changamoto za maji katika wilaya ya Bahi ambapo watanufaika na bomba la maji kupitia gridi ya maji ya Taifa kutoka ziwa Victoria kwa ajili ya matumizi ya majumbani, kilimo na ufugaji.
SGR
Mhe. Samia amewaahidi wananchi wa jimbo la Bahi kunufaika na mradi wa SGR katika awamu ya pili na ya tatu ambapo kwa kiwango kikubwa itabadilisha kabisa taswira ya Uchumi katika wilaya ya Bahi hususani kwa vijana.
Sambamba na hili ameahidi kuwalipa fidia wananchi waliopisha mradi wa SGR.
KILIMO
Mgombea wa Urais amesema kuwa mengi yamefanyika katika kipindi cha uongozi uliomalizika katika kuinua sekta ya kilimo ikiwemo ya ujenzi wa skimu ya umwagiliaji maji.
Amesema katika kipindi kijacho serikali yake itaanzisha mashamba makubwa ambayo ni Chibelele, Msisi, Ibugule, babayu,mondumu na Zanka ili kuwawezesha vijana ili kuinua vipato vyao.
MIUNDOMBINU
Kuhusu miundombinu ya Barabara Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa serikali yake katika kipindi cha miaka minne serikali imefanya mengi ya kujenga miundombuni ya Barabara, hata hivyo anatambua changamoto bado zipo ikiwemo ya Barabara ya mwanachungu – Bahi - Sokoni- SGR (km 6) ambapo ameahidi kujengwa kwa awamu mbili.
Awamu ya kwanza ni kujenga Daraja na mto Mkogwa ambapo usanifu umekamilika na kisha ujenzi wa Barabara yenyewe.
VIWANDA
Kuhusu sekta ya Viwanda ametoa ahadi kwa wananchi wa Bahi kuwa endapo atachaguliwa tena kwa muhula wa pili atahakikisha anajenga kongani ya viwanda ili kuongeza thamani ya bidhaa mbalimbali zinazozalishwa kwenye wilaya ya Bahi ambayo itaongeza ajira kwa vijana.
