Mgombea wa Urais kupitia CCM Dkt Samia Suluhu Hassan ameendelea na ziara za kampeni za uchaguzi mkuu wa 2025 ambapo jana tarehe 6 Septemba 2025 amefanya mikutano ya kampeni katika wilaya tofauti, ambapo wakati akiwahutubia wananchi wa Makambako, Dkt. Samia alisema amekuja kuomba kura kutokana na mambo mawili: kwanza, yale ambayo serikali ya CCM imeyafanya katika kipindi kilichopita, na pili, yale yaliyopangwa kutekelezwa katika Ilani ya 2025-30.
Alisisitiza kuwa kazi ya viongozi wa chama ni kupita na kuwaeleza wananchi mafanikio yaliyopatikana na mipango iliyoko mbele.
Aidha, ameeleza kuwa tayari serikali inafungua vituo 8 vya kununua mahindi ndani ya Mkoa wa Njombe ili wakulima wapate masoko ya uhakika ya mazao yao. Mbunge wa jimbo aliomba kukabidhi andiko la mradi wa umeme wa upepo na Dkt. Samia alisisitiza kuwa wasaidizi wake wako tayari kupokea na kuufanyia kazi, kwani mradi huo unaendana na ajenda ya Nishati Safi.
Aliahidi pia kuanzishwa kwa One Stop Center Makambako ili kuwa mji mkuu wa biashara, ambapo timu imeundwa kushughulikia marekebisho ya mifumo ya kodi na urasimu wa nyaraka. Pia ameeleza kuwa maombi ya kuanzisha bandari kavu yataangaliwa.
Kuhusu elimu ya juu, alisisitiza kuwa maandalizi ya ujenzi wa Chuo cha Mwalimu Nyerere yamekamilika na serikali itagharamia ujenzi huo.
Vilevile, aliwahakikishia wananchi kuwa ombi la Makambako kuwa wilaya litaangaliwa katika awamu ijayo.
IRINGA
Akizungumza na wananchi wa Mufindi, Dkt. Samia aliwashukuru kwa kujitokeza kwa wingi, jambo linaloonyesha imani yao kwa CCM na wagombea wake.
Amesema katika miaka mitano iliyopita, miradi mingi ya maendeleo imetekelezwa, na wabunge wao wataendelea kuwaeleza wananchi miradi hiyo.
Kipaumbele kikubwa, alisema, ni miundombinu ya barabara, ikiwemo barabara ya Nyororo–Mtwango yenye urefu wa km 40.4 ambapo mkandarasi yupo site na kazi inaendelea.
Pia barabara ya Igowelo–Kasanga–Nyigo (km 54.5) itafanyiwa kazi.
Ameeleza kuwa ombi la mashine ya X-Ray tayari linafanyiwa kazi na huduma hiyo inakuja katika hospitali ya wilaya. Kuhusu madai ya kiwanda cha Mgololo, alisema hapo zamani serikali na mwekezaji walishalipa madai lakini kumetokea madai mapya, na sasa serikali inafanyia tathmini upya ili malipo halali yalipwe.
Aidha, kuhusu kiwanda
cha chai cha Mufindi (cha DL), alisema inawezekana mwekezaji alipitia changamoto za kibiashara lakini sasa amepata mkopo kutoka benki za Tanzania takribani shilingi bilioni 2.7, na ameanza kulipa.
Aliongeza kuwa fedha za kufufua kiwanda na kununua mashine mpya za uzalishaji zimepatikana, na kama mwekezaji atashindwa, serikali itaingilia kati kuchukua mashamba chini ya vyama vya ushirika ili viendelee kuendelezwa.
Alisisitiza kuwa huduma za kijamii kama elimu, afya, maji na umeme ni haki ya kila mwananchi na serikali ya CCM itaendelea kuzisogeza karibu na wananchi.
Kila mtoto ataenda shule hadi kidato cha sita, na wanafunzi wa vyuo vikuu watakuta mikopo tayari ipo.
MAFINGA
Katika mkutano uliofanyika Mafinga, Dkt. Samia alishukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi na kusema kuwa umati huo unaonyesha kuwa Mafinga imewaka kijani cha Chama Cha Mapinduzi.
Aliahidi kuendeleza kasi ya maendeleo katika miaka mitano ijayo kwa kuzingatia sekta kuu za elimu, afya, maji na umeme.
Aidha, alisema ujenzi wa miundombinu ya barabara ni kipaumbele kikubwa, ili kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa. Alisisitiza kuwa hata kama barabara zote hazitakamilika awamu ijayo, serikali itahakikisha kazi kubwa ya ujenzi inafanyika katika kila wilaya.
Katika sekta ya viwanda, alisema serikali itaweka kongani za viwanda kulingana na mazao yaliyopo, hasa katika misitu na kilimo, ili kufikia soko la kimataifa. Aliongeza kuwa ruzuku za kilimo, pembejeo na mbegu bora zitaendelea kutolewa, sambamba na ruzuku ya chanjo kwa mifugo. Amesisitiza kuwa lengo la CCM ni kuhakikisha Tanzania inazalisha chakula na mazao ya biashara kwa wingi, na tayari mauzo ya mahindi yameanza katika nchi jirani.
Kwa upande wa masoko, alisema serikali imeanza kununua mahindi Ruvuma na Rukwa, na sasa vituo vya kununua mazao vitafunguliwa pia Njombe, Iringa na Mbeya. Aidha, aliahidi kujenga stand mpya ya kimataifa Mafinga ili kuboresha usafirishaji na biashara.
4. KALENGA – IRINGA VIJIJINI
Katika mkutano uliofanyika Kalenga, Dkt. Samia aliwashukuru wananchi kwa mapokezi na ukarimu wao mkubwa. Amesema lengo la CCM ni kujenga taifa lenye uchumi jumuishi na linalojitegemea, huku akisisitiza kuwa maendeleo yanayogusa maisha ya mwananchi mdogo ndiyo yanayojenga taifa imara.
Amesema umeme umefika vijijini na maji yanasambazwa, shule mpya zimejengwa na mtoto wa mkulima sasa anasoma shule nzuri.
Hayo, alisema, ndiyo maana halisi ya kumjali mnyonge – si maneno tu.
Kuhusu miradi ya miundombinu, alisema tayari bajeti imetengwa kwaajili ya mradi wa Makumbusho-Kalenga na mkandarasi atakuwa site hivi karibuni.
Aidha, mtandao wa barabara za lami umeongezwa kwa km 32 na changarawe km 191, huku madaraja 34 yakiwa yamejengwa.
Ameahidi pia kujenga daraja katika kijiji cha Maperamengi ili kurahisisha usafiri unawezekana wakati wa mvua, na daraja la Kitwiru–Isakalilo litajengwa katika awamu ya pili ya mpango wa TACTIC.
Kuhusu mabwawa, alisema tayari mitambo imenunuliwa na katika awamu ya sita ya pili mabwawa mapya yatachimbwa Kalenga na maeneo mengine.
Amehitimisha kwa kutoa wito kwa wananchi wa Kalenga na Iringa kwa ujumla kuendeleza mapambano ya kujenga maendeleo ya Tanzania kwa kuchagua CCM.
