Mgombea wa Urais wa CCM, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipokelewa kwa shangwe kubwa Tukuyu Mjini.
Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ameambatana wa viongozi mbalimbali wa kitaifa wa CCM akiwemo Katibu Mkuu Mhe. Dkt. Asha-Rose Migoro na Katibu wa itikadi na uenezi Kenan Kihongosi na viongozi wengine wa chama wa mkoa na wilaya.
Mhe.Dkt. Samia alisisitiza kuwa dhamira ya CCM ni kuhakikisha kila kijiji na kila kitongoji kinapata huduma bora za msingi.
Kama kuna shida ya maji, miradi ya maji vijijini italetwa na umeme,vijiji vimeshaunganishwa na sasa huduma inasogea katika kila kitongoji ili kila kayaipate umeme. Aidha, shule na vituo vya afya vinaendelea kujengwa vijijini kwa ubora wa hali ya juu ili wananchi wapate huduma karibu.
Akizungumzia sekta ya kilimo na mazao ya biashara, Dkt. Samia alitumia muda kueleza kuhusu zao la chai na parachichi.
Kuhusu chai, alieleza kuwamashamba yaliyokabidhiwa kwa wawekezaji binafsi kama WATCO na MOHAMED ENTERPRISES yalitolewa kwa imani kuwa yataendeleza sekta hiyo.
Serikali iliweka mazingira rafiki ya uwekezaji, ikiwemo sera, sheria na miundombinu ya maji na umeme.
Hata hivyo, changamoto zimejitokeza, na hivyo serikali imeunda timu maalumu ya kufanya tathmini ya mashamba na viwanda vya chai. Lengo ni kuhakikisha mashamba hayo yanamilikishwa kwa vyama vya ushirika chini ya uongozi wa serikali, ili kuongeza thamani ya chaikabla ya kusafirishwa.
Aidha, alisisitiza kuwa serikali imetoa maelekezo kwa wawekezaji waliopo
kulipa madeni yao kwa wakulima na wafanyakazi wa viwanda, kabla serikali
haijachukua hatua ya kuhamisha umiliki. Aliwaahidi wananchi wa Rungwe
kwamba madeni hayo yatalipwa katika kipindi kifupi atakapochaguliwa tena
kuliongoza taifa letu.
Kuhusu zao la parachichi, Dkt. Samia alifafanua kuwa zao hilo sasa lina soko
kubwa duniani, na Tanzania inashika nafasi ya tatu barani Afrika kwa kuzalisha
parachichi bora. Changamoto inayokumba sekta hii ni kushuka kwa bei,
jambo linalowavunja moyo wawekezaji. Hata hivyo, serikali ya CCM
imepanga kujenga vituo 50 vya kuhifadhi parachichi na mbogamboga, viwili
kati ya hivyo vitajengwa Rungwe. Vituo hivyo vitasaidia kuhifadhi mazao kwamiezi mitatu, ili wakulima wasiuze kwa bei ya hasara, bali wasubiri soko liwe juu.
Katika hatua nyingine Dkt Samia amesema , kupitia mpango wa kongani za viwanda na programu ya BBT, serikali atakayoiunda itawekeza kwenye viwanda vya vijana vitakavyoongeza thamani ya parachichi. Parachichi ambazo zitaharibika zitatumika kutengeneza bidhaa nyingine kama mafuta ya parachichi, chakula cha mifugo na bidhaa mbalimbali za viwandani. Ili kuendeleza zao hili, serikali imeamua kuwaajiri maafisa ugani watakaowasaidia kupima afya ya udongo na kuwapatia maarifa bora ya kilimo, pamoja na kutoa pembejeo na huduma za ugani. Dkt. Samia alisisitiza kuwa ruzuku ya serikali itaendelea, ikiwemo mbolea na dawa za kupulizia, ili kuongeza tija na kuhakikisha zao la parachichi linakuwa nguzo ya uchumi wa wananchi wa Rungwe.
MBARALI Kwenye mkutano wake wa pili Mbarali, Mgombea wa Urais wa CCM, Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliwashukuru wananchi wa Mbarali kwa mapokezi
makubwa na imani yao kwa CCM na kusisitiza kwamba Mkoa wa Mbeya
umewaka kijani. Aliwapongeza viongozi wa CCM kwa kazi kubwa waliyofanya
na kuwakumbusha wananchi kwamba miaka mitano iliyopita, serikali ya CCM
imetekeleza mikakati mingi ya kimaendeleo katika sekta zote muhimu.
Kuhusu sekta ya afya, wilaya ya mbarali, alibainisha kwamba hospitali moja
ya wilaya imejengwa, vituo vya afya vinne na zahanati tisa zimeongezwa.
Vifaa tiba na watumishi wamepelekwa, na sasa wananchi wanapata vipimo
na huduma muhimu kwenye hospitali ya wilaya. Kwenye elimu, shule mpya za
msingi 35 na sekondari 14 zimejengwa, sambamba na kuongeza walimu na madarasa kwenye shule zilizopo ili kupunguza msongamano wa wanafunzi.
Kwa upande wa maji, serikali imetenga shilingi bilioni 10 kupitia RUWASA kwa ajili ya visima 30. Aidha, miradi 11 ya maji kutoka vyanzo vya mito na matanki mawili ya kuvuna maji ya mvua imetekelezwa. Zaidi ya shilingi bilioni 51.5 zimeelekezwa kwenye mradi mkubwa wa maji wa miji 28, ambao utawafaidisha wananchi wengi wa Mbarali kupata maji safi na salama.
Dkt. Samia alikumbusha kuwa baada ya kuhakikisha vijiji vyote vya wilaya ya Mbarali vimeunganishwa na umeme, sasa serikali inaendelea kumalizia vitongoji.
Kati ya vitongoji 712, tayari 641 vimeunganishwa na huduma hiyo, na ameahidi kumalizia vilivyosalia ili kila kaya ifikie maendeleo.
Sekta ya miundombinu pia imepewa kipaumbele, ambapo zaidi ya shilingi bilioni 11 zimetumika kujenga barabara za lami kupitia TARURA, pamoja na madaraja manne. Zaidi ya kilomita 464.5 za barabara za changarawe zimeboreshwa ili kuhakikisha zinapitika mwaka mzima. Aidha, alieleza umuhimu wa kuhamisha vijiji vitano vilivyokuwa ndani ya Hifadhi ya Ruaha, kwani hifadhi hiyo ndiyo chanzo cha maji kinachozalisha umeme Mtera na Kidatu.
Alisisitiza kuwa bila kulinda hifadhi hiyo, taifa lingekabiliwa na upungufu mkubwa wa umeme.
Kuhusu fidia, aliwahakikishia wananchi kwamba tathmini ya madai ya fidia kwa walioathirika itakamilishwa ili wote walipwe.
Aliongeza kuwa serikali imeamua kununua shamba la uwekezaji la Mbarali Estate kwa ajili ya kuligawa kwa wananchi, kutokana na changamoto ya ufinyu wa mashamba.
Akitoa mwelekeo wa awamu inayofuata, Dkt. Samia aliahidi kukamilisha miradi yote ya maji safi na salama, kujenga barabara za mitaa kwa kiwango cha lami, ikiwemo barabara ya Kagomba–Ukaguzi na Utego kuelekea viwandani.
Aidha, mtandao wa barabara za lami utaendelezwa katika maeneo ya Igava, Lujewa, Ubaruku, Chimala, Igurusi, Majimbila na Kapunga, kuhakikisha wananchi wanapata barabara bora za kisasa.
Kwa dhamira ya kujenga Tanzania inayojitegemea, alisisitiza kuwa kila mradi utakaoanzishwa Mbarali utamalizika kwa wakati na kwa ubora, na wakati huo huo miradi mipya itaendelea kuanzishwa na kukamilishwa. Aidha, alisema serikali itaimarisha mifumo yake ya utendaji ili wananchi wa Mbarali waweze kufanya kazi zao kwa bidii, weledi na mafanikio, bila vikwazo vya huduma za msingi.

