TANGAZO

TANGAZO

KURA NI HAKI, AMANI NI MSINGI : WAJIBU WA KILA MTANZANIA KUELEKEA OKTOBA 29


Na. Mwandishi wetu

 Tukiwa tunakaribia Uchaguzi Mkuu, wito mkubwa unatolewa kwa Watanzania wote kulinda hazina yetu ya Amani na Utulivu. 

Demokrasia haina maana bila amani. Kila mmoja wetu ana wajibu wa kuhakikisha kuwa, licha ya tofauti zetu za kisiasa, tunadumisha heshima, tunafanya siasa safi, na tunakubali matokeo yanayotokana na sanduku la kura. 

Tukumbuke kwamba nchi yetu ni moja, na upigaji kura ni zoezi la muda mfupi, lakini amani ni urithi wa kudumu kwa vizazi vijavyo.

Mmoja wa waimbaji wa Injili Christina Shusho ambaye alishawahi kuwa katika kamati ya Amani nchini Tanzania wakati wa Utawala wa awamu ya nne anasema kwamba kila siku ni lazima wananchi lazima watambue umuhimu wa uhai na kuenzi Amani.

Anasema ni kazi kubwa kuenzi Amani lakini ni rahisi kubomoa kama watu hawatakuwa waangalifu katika kauli na matendo yao na kwamba bila Amani hakuna shughuli nyoiyote itakayostawi.

Uchaguzi Sio Vita, Ni Maamuzi

Ni muhimu kwa Vyama vya Siasa na Wafuasi wao kuweka mbele maslahi ya Taifa. Uchaguzi si vita, bali ni mchakato wa kidemokrasia wa kuchagua viongozi tunaowaamini. Badala ya kuruhusu jazba na chuki, tunapaswa kujikita katika hoja, mijadala yenye tija, na kufuata sheria na taratibu zilizowekwa. 

Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi vimeapa kulinda raia na mali zao, na vinahitaji ushirikiano wetu ili kudumisha utulivu katika kipindi chote cha kampeni, upigaji kura na baada ya matokeo. Tutumie fursa hii ya kidemokrasia kwa ustaarabu na utulivu.

Jukumu la Kiongozi na Mwananchi

Viongozi wa kisiasa wanalo jukumu la kutoa hotuba zenye kuhamasisha umoja na kuacha kauli zinazochochea mgawanyiko au vurugu. Kadhalika, kila mwananchi anawajibika kuepuka kueneza taarifa za upotoshaji (fake news) au uchochezi kupitia mitandao ya kijamii. Amani huanzia kwetu. 

Kanisa Katoliki kupitia viongozi wake wakuu akiwemo Askofu Mkuu wa jimbo kuu la Dar es Salaam Thadeus Ruwaich amesisitiza wananchi kutoyumbishwa na taarifa zisizo sahihi na kwamba kanisa halina ugomvi na serikali na ni vyema wananchi wakatimiza sharia zilizopo.

Kwa kuhakikisha kila hatua ya uchaguzi inakwenda kwa utulivu, Watanzania wanapaswa kutoaa heshima kwa katiba ambayo ndiyo inaweka msingi thabiti wa maendeleo endelevu. Tanzania itabaki salama na imara ikiwa wananchi wataweka kura zao kama haki yao, na amani kama wajibu wao.

TANZANIA SASA INA TAKWIMU ZA MAENDELEO ZINAZOPIMIKA 

Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, na chama chake wamefanikiwa kudhihirisha wazi kwamba wanatosha na wameiandaa Tanzania kwa hatua kubwa inayofuata ya maendeleo, huku wakikabiliana na wapotoshaji wachache kwa kutumia lugha moja tu: Matokeo Yanayopimika.

Tukielekea Uchaguzi Mkuu, kuna jambo moja lisilopingika: Ukweli hauwezi kufichwa. Wanaojaribu kufunika jitihada kubwa za maendeleo nchini wamejikuta wakiumia kwa sababu jua la mafanikio linaangaza kila kona ya taifa.

Dkt. Samia alikabidhiwa nchi wakati ikiwa kwenye majonzi, lakini badala ya kutetereka, alisimama imara. Ameiweka Tanzania katika viwango vipya vya uongozi vinavyopimika si kwa maneno matupu, bali kwa takwimu na matokeo yanayoonekana kwa macho.

Mageuzi Makubwa katika Nishati na Elimu

Chini ya uongozi wake, sekta ya Nishati imeshuhudia mabadiliko makubwa. Uzalishaji wa umeme nchini umeongezeka kutoka megawati 1,602 mwaka 2020 hadi kufikia megawati 3,078 mwaka 2024. Ongezeko hili kubwa, ambalo linatokana kwa kiasi kikubwa na mradi wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP), linatoa uhakika wa umeme wa kutosha kwa viwanda na matumizi ya nyumbani.

Sambamba na hilo, dhamira ya kupeleka umeme hadi vijijini imeimarika, ambapo vijiji vyenye umeme vimeongezeka kutoka 8,587 mwaka 2020 hadi kufikia 12,318 mwaka 2024. Hii ni ishara ya wazi ya kuondoa giza na kupeleka maendeleo kwa wananchi wa hali ya chini.

Katika sekta ya Elimu, namba zinaonesha ari mpya. Idadi ya shule za msingi imeongezeka kutoka 16,656 mwaka 2020 hadi 19,783 mwaka 2024, huku shule za sekondari zikipanda kutoka 5,000 hadi 5,929. Hatua hii inahakikisha watoto wa Kitanzania wanapata nafasi za kutosha za elimu bora kuanzia chini hadi juu.

Afya na Uchumi wa Mwananchi Zaimarishwa

Uboreshaji wa sekta ya Afya pia umekuwa kipaumbele. Upatikanaji wa dawa na vifaa tiba umeimarika kutoka asilimia 75.6% mwaka 2020 hadi asilimia ya kuvutia ya 89.3%, hatua inayoimarisha huduma za afya nchini kote.

Katika kusaidia wananchi wengi, Serikali imewekeza katika sekta za uzalishaji. Matumizi ya mbolea kwenye Kilimo yameongezeka kutoka tani 586,604 mwaka 2020 hadi zaidi ya milioni 1.2 mwaka 2024. Aidha, eneo linalotumia umwagiliaji limepanda kwa kasi kutoka hekta 561,383 hadi 983,466, hatua muhimu ya kuifanya kilimo kisitegemee mvua.

Katika sekta ya Uvuvi, wavuvi wamewezeshwa kwa ongezeko la boti za kisasa kutoka 280 mwaka 2020 hadi 507 mwaka 2024, na hivyo kuongeza tija na kipato chao.

Propaganda Zatafunwa na Ukweli

Haya yote ni ushahidi wa dhahiri kwamba Mama Samia si kiongozi wa maneno, bali wa matokeo ya kweli. Wanaojaribu kupotosha ukweli huu wanapaswa kuelewa kuwa Tanzania ipo kwenye njia ya maendeleo isiyozuilika.

Kazi na utekelezaji vinafanywa kwa vitendo, na jitihada zozote za kutumia propaganda za kisiasa kuzuia safari hii zitakumbana na ukweli wa takwimu hizi. Ukweli unaendelea kuangaza – na ukweli huo ni huu: Mama Samia ameahidi, na ametekeleza.

MSIMAMO WA KIJANA: Kama Nilijiandikisha, Kwanini Nisipige Kura Oktoba 29? 

Na Mwandishi wetu

Wakati taifa likielekea kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, mjadala mkali umeibuka miongoni mwa vijana kuhusu umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika upigaji kura. Mfumo wa kidemokrasia unasisitiza kuwa Kura yako ni haki yako ya msingi, na usipopiga kura utachaguliwa viongozi, lakini bado kuna kundi kubwa la vijana linaelekea kukaa kimya.

Hoja iliyoibuliwa hivi karibuni na mmoja wa vijana, Said Nassoro ambaye ana makazi yake Kawe.

"Kama nilienda kusimama foleni kujiandikisha daftari la kudumu, kwanini Oktoba 29 nisiende kupiga kura?" Swali hili linafungua mjadala kuhusu utofauti kati ya kujiandikisha na kupiga kura na kwanini vijana wanahitaji kukamilisha hatua ya mwisho.

Sababu za Vijana Kukaa Kimya

Licha ya uhamasishaji mkubwa kutoka kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na wadau wengine kuna wimbi mtandaoni lin alohimiza vijana kutoshiriki uchaguzi wakimezeshwa taarifa za uongo kuhusu michakato ya uchaguzi.

Wachambuzi wa mitandaoni wanasema japo idadi ni ndogo lakini vijana wanaweza kirahisi kupotoshwa na taarifa za uongo kuhusu michakato ya uchaguzi, jambo linaloweza kuwafanya waamini kuwa upigaji kura hauna maana.

Nassoro anasisitiza kuwa kujiandikisha ni ishara ya kwanza ya utayari wa kiraia, lakini kukamilisha zoezi kwa kupiga kura ndio uamuzi mkuu unaohitajika.

"Kama ulikuwa na nia njema ya kuchagua kiongozi, kwanini ufanye safari ya nusu kwa kujitokeza kwenye Daftari, halafu ukatae kukamilisha kwa kutumia kura yako? Kura yangu ina maamuzi. Inasaidia kwenye mjadala mtandaoni. Badala ya kulalamika baada ya uchaguzi, ni bora kutumia sekunde chache kwenye sanduku la kura."

Kina anaungwa mkono na Joshua Atanazi, kijana mwingine, ambaye alisema: "Kundi la vijana lina idadi kubwa nchini na ndiyo lenye nafasi ya kufanya mabadiliko chanya kupitia kura zao. Usipopiga kura, kesho usilalamike."

INEC Yasimama Kidete

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) inaendelea kuhimiza vijana na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi. Kaulimbiu yao inabaki: "UCHAGUZI MKUU OKTOBA 29, 2025. Kura Yako Haki Yako Jitokeze Kupiga Kura."

Kwa mujibu wa Tume, upigaji kura ni hatua muhimu ya kutimiza wajibu wa kiraia na ndio msingi wa kuwa na haki ya kuwawajibisha viongozi baada ya uchaguzi. Taasisi za dini nchini pia zimehimiza waumini kuombea taifa na kushiriki katika zoezi hilo la kidemokrasia kwa amani.

Uchaguzi huu unawaweka vijana katika njia panda: ama waache sauti yao ipotee kwa kukaa kimya, au waitumie kura yao kama kifaa cha kuamua nani anastahili kuongoza taifa kwa miaka mitano ijayo. Jibu la swali la Nassoro, kwa mujibu wa INEC na wadau, ni wazi: Usiache kura yako iishe kwenye foleni ya kujiandikisha.

KUWAITA WASTAAFU: KUREJESHA UZOEFU, SI NJAMA YA KISIASA

Na Mwandishi wetu

Katikati ya mijadala ya kisiasa inayoendelea kuelekea uchaguzi, hatua ya Serikali ya kuwaita baadhi ya maafisa wa Jeshi la Polisi walio staafu kurejea kazini kwa mkataba imejikuta ikivutwa kwenye dimbwi la siasa na kupotosha. Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya usalama wanasisitiza kuwa utaratibu huu si jambo geni na unalenga kujaza ombwe la utaalamu na uzoefu unaohitajika katika kipindi hiki nyeti.

Kiapo cha Utii Kinabaki Hai

Kwa mujibu wa wataalamu wa menejimenti ya vikosi vya usalama, madai kwamba kurejeshwa kazini kwa wastaafu kunaashiria njama au udhaifu wa kiusalama hayana msingi wa kiutawala wala kisheria. Kimsingi, askari wa Tanzania huchukua kiapo cha utii na uaminifu kwa Taifa ambacho, kisheria, kinabaki hai hata baada ya kustaafu.

Kiapo hiki huruhusu askari hao kuitwa tena kazini kulingana na mahitaji maalum ya kitaifa ili kutoa nguvu kazi au uzoefu wa ziada. Hatua hii huonekana katika nchi nyingi duniani, hasa katika taasisi zinazohitaji utaalamu usiopatikana kwa urahisi, kama vile jeshi na polisi.

Uzoefu Muhimu Katika Ulinzi wa Uchaguzi

Taarifa za ndani ya Jeshi la Polisi zinaeleza kuwa kuitwa kwa askari hawa wastaafu, ambao wengi wao wana uzoefu mkubwa katika kulinda usalama na amani wakati wa chaguzi zilizopita, ni utaratibu wa kujenga uwezo wa kiutendaji.

Jukumu kuu la Jeshi la Polisi wakati wa uchaguzi ni kulinda raia na mali zao, kulinda masanduku ya kura, na kuhakikisha amani inakuwepo. Kwa hiyo, kiongezeko chochote cha nguvu kazi ya ulinzi, hasa kutoka kwa watu wenye uzoefu wa muda mrefu, kinalenga kuimarisha amani hiyo na utulivu wa mchakato, na si kuuvuruga.

Kudhibiti Siasa za Upotoshaji

Jaribio la kutafsiri utaratibu huu wa kawaida wa kiutawala—kuajiri wataalamu wastaafu kwa mkataba kutokana na uhitaji—kama propaganda ya chuki au hofu ni hatua ya kisiasa inayolenga kutafuta kasoro hata katika hatua za msingi za ulinzi wa Taifa.

Ukweli wa amani na utulivu wa Watanzania haubadiliki kwa sababu ya taarifa za kupotosha. Tanzania ina mfumo wa ulinzi unaoheshimu sheria. Kufanya siasa kwa kutumia mbinu za kuchochea hofu kuhusu usalama wa uchaguzi kunakumbana na ukweli wa utaratibu uliowekwa kisheria wa Serikali wa kutumia uzoefu wa watumishi wake wa zamani. Watanzania wengi wanajua thamani ya amani na hawatadanganywa kwa urahisi.

Kama una Taarifa,Picha, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kwa simu +255 766 166 125 au Email : emmymwaipopo@gmail.com