Akizungumza baada ya kukagua na kujionea utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika bandari ya Dar es Salaam, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema kina cha bandari kimeongezwa hadi kufikia mita 15, hatua inayowezesha bandari hiyo kupokea meli kubwa na ndefu zaidi zenye urefu wa zaidi ya mita 300 na uwezo mkubwa wa kubeba mizigo.
Msigwa amesema maboresho hayo yamepunguza kwa kiasi kikubwa gharama za usafirishaji na uendeshaji wa biashara, huku yakiongeza uwezo wa bandari hiyo kuhudumia na nchi jirani.
Aidha amebainisha kuwa kuongezeka kwa uwezo wa bandari ya Dar es Salaam kumeifanya Tanzania kuwa lango muhimu la biashara kwa nchi za Zambia, Burundi, Rwanda, Malawi na Uganda, ambapo kwa upande wa Zambia, tani zaidi ya Mil.3 za mizigo zimehudumiwa, zaidi ya tani laki nne kwa Burundi, pamoja na shehena kubwa kutoka Rwanda, Malawi na Uganda.
"Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) iliingia mkataba wa upangishaji na uendeshaji wa bandari na makampuni ya DP World na TEAGTL, hatua iliyochochea uwekezaji mkubwa wa kisasa.
Tangu kuingia kwa mkataba huo, DP World imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 214.2 huku uwekezaji kutoka kampuni ya TEAGTL umeweka zaidi ya shilingi Bil. 410.4 Kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ambapo uwekezaji huo umeleta mafanikio makubwa ikiwemo kununua mitambo mipya ya kupakia na kupakua mizigo, kuboresha maeneo ya kuhifadhi makontena, pamoja na kufanya ukarabati wa karakana na mitambo mbalimbali.
Aidha, Msigwa ameongeza kuwa, gharama za uendeshaji wa TPA umeshuka kwa zaidi ya asilimia 57, huku mapato yatokanayo na forodha yakifikia zaidi ya shilingi trilioni 12.3, hatua inayochangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza uchumi wa taifa.

