Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ametoa wito kwa viongozi wa Majukwaa ya Uwezeshaji Wanaume nchini kuimarisha ushiriki wao ili kukuza usawa wa kijinsia na ustawi wa jamii kwa ujumla.
Akizungumza katika mkutano na Viongozi wa Majukwaa ya Wanaume wa Mkoa wa Dodoma Januari 23, 2023 jijini Dodoma, Waziri Gwajima amesema ushiriki wa wanaume ni nguzo muhimu katika kufanikisha malengo ya Sera ya Taifa ya Jinsia ya mwaka 2023 na maendeleo jumuishi ya Taifa, ambayo imeweka mkazo kwenye ushirikishwaji wa wanaume katika masuala ya kijamii, kiuchumi, kimazingira na kitamaduni.
“Wanaume mna nafasi kubwa katika ustawi na maendeleo ya jamii. Sera ya Taifa ya Jinsia ya mwaka 2023 inasisitiza umuhimu wa mwanaume kama mhimili wa mabadiliko na uendelevu wa familia. Ushiriki mdogo wa wanaume katika masuala ya kijinsia unaendelea kudhoofisha jitihada za Serikali na wadau katika kujenga jamii yenye usawa. Ni wakati wa wanaume kuwa sehemu ya suluhisho,” amesema Waziri Gwajima.
Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amewahimiza viongozi wa majukwaa ya wanaume kutoka mikoa mbalimbali nchini kuchukua nafasi yao kikamilifu katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na ubaguzi wa aina zote na kusisitiza kuwa usawa wa kijinsia hauwezi kufikiwa bila ushiriki wa wanaume.
Wanaume ni wadau muhimu katika kubadilisha mitazamo hasi iliyojengeka katika jamii, Mhakikishe mnatumia majukwaa ya kidijitali kutoa elimu na kuhamasisha uwajibikaji wa wanaume ndani ya familia na kushiriki katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, malezi bora ya watoto na ulinzi wa maadili na tunu za Taifa. Ni matumaini yangu mtakuwa mabalozi wa mabadiliko katika maeneo yenu na kushirikiana na serikali, asasi za kiraia na wadau wa maendeleo, ili kujenga jamii salama, jumuishi na yenye fursa sawa kwa wanawake, wanaume na makundi maalum”, amesisitiza Waziri Gwajima.
Aidha, Waziri Gwajima amewapongeza viongozi wa majukwaa ya wanaume kwa jitihada zao na kuwataka kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutekeleza maono ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, yaliyoainishwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ya kuhakikisha maendeleo jumuishi kwa wananchi wote.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanaume mkoa wa Dodoma, Peter Mavunde meeleza dhumuni la kuwanzishwa majukuwaa haya ni kuwa na chombo kitakachounganisha wanaume wote pamoja kwa ajili ya kujulishana fursa na kujadili namna ya kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.
“Tuna malengo ya kuandaa muongozo wa uratibu wa Majukwaa ya Uwezeshwaji Wanaume kiuchumi ambao utatumika kuratibu majukwaa hayo Tanzania nzima, pamoja na kutayarisha muundo utakaotumika kuendesha na kuboresha majukwaa kuanzia ngazi ya Mkoa, wilaya, Kata, vijiji na vitongoji ili wanaume wote waweze kushiriki”, amesema Mavunde.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Viongozi mbalimbali kutoka awizarani akiwemo Naibu Katibu Mkuu Wakili Amon Mpanju anayeshughulikia Makundi Maalum, viongozi wa majukwaa ya wanaume kutoka mikoa mbalimbali waliyoshiriki kwa njia ya mtandao, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Mikoa na wadau wengine.

