Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeyapatia ufumbuzi malalamiko ya muda mrefu ya viwanja mbadala kwa wananchi wa jiji la Dodoma.
Suluhisho hilo linafuatia malalamiko ya takriban wananchi 4000 wa jiji la Dodoma wanaodai viwanja na halmashauri ya jiji la Dodoma kuwapa ahadi bila kutekeleza mpaka sasa.
Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 25 Februari 2026 na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo wakati akizungumza na wananchi wenye migogoro ya ardhi katika eneo la Mahomanyika lilopo kata ya Nzuguni jijini Dodoma.
Dkt Akwilapo amesema, eneo la Mahomanyika ni eneo la serikali hivyo lipangwe na kupimwa kwa ajili ya utatuzi wa migogoro ya meneo mbalimbali ya jiji la Dodoma pamoja na matumizi ya serikali.
"Eneo hili lenye mgogoro hapa Mahomanyika ni eneo la serikali hivyo lipangwe na kupimwa kwa ajili ya utatuzi wa migogoro na siyo ya hapa tu na mingine ya jiji la Dodoma na matumizi ya serikali" amesema.
Amesisitiza kuwa katika upangaji wa eneo hilo kipaumbele kiwe kutatua changamoto za wananchi wa jiji la Dodoma ambao kwa muda mrefu wamedai viwanja na jiji kuwaahidi bila ya kuwapatia.
Katika kufanikisha zoezi hilo, zimeundwa timu mbili kwa ajili ya upangaji na upimaji na pamoja na ile ya kushughulika na uhakiki wa wananchi wenye migogoro na kustahili kupatiwa viwanja mbadala.
"Timu hizi zitaanza kazi mara moja na kazi hiyo itafanyika kwa muda wa siku sitini, miezi miwili kazi iwe imekamilika kila mtu kujua amepata nini na anaenda wapi" amesema.
Akigeukia uuzwaji viwanja 1,037 vilivyoingizwa kwenye mfumo wa TAUSI ili wananchi wapate viwanja vilivyopimwa katika eneo la Mahomanyika, Dkt. Akwilapo amuagiza Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma kuendelea na uuzaji viwanja kwa waombaji 352 pekee walioanza kulipa huku wale ambao hawajaanza kulipa maombi yao yasitishwe.
Eneo la Mahomanyika limekuwa na changamoto ya malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wananchi wakidai ni wamiliki wa asili wa maeneo hayo jambo lililosababisha kuundwa kwa Timu (Timu ya DC) ambayo ilishirikisha wananchi, Vyombo vya Usalama na Wataalam ambapo timu hiyo ilibaini eneo husika ni eneo la Serikali.




