Waswahili husema mwenda kimya ndio mla nyama , ndivyo alikuwa faru Vicky anayepatikana ndani ya hifadhi ya Ngorongoro.
Ukimya na utulivu wa faru Vicky ulimfanya kuwa kimbilio la madume wengi kwa kuwa waliamini Vicky ni jike mwenye malengo na anayejali faru madume.
Faru Vicky alizaliwa mwaka 1975 na kukulia ndani ya kasoko ya Ngorongoro ambapo mama yake aliitwa faru Anna, baba yake hakujulikana kutokana na tabia za faru Anna kutembea na madume mengi katika Kasoko hiyo.
Kwa mujibu wa daktari wa wanyama wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Dkt Dickson Wambura, Faru Vicky hakuwa na mbwembwe nyingi alikuwa mtulivu na hakuwa na tabia ya kuzunguka zunguka ovyo hifadhini.
Dkt Wambura anaeleza kuwa faru Vicky alitumia mda mwingi ndani ya Kreta ya Ngorongoro huku midume ikijigonga kila mmoja akitaka awe naye hata hivyo wenye nguvu na akili ndiyo walimpata.
Alikulia ndani ya kreta hadi alipofikia umri wa kuachana na mama yake na kuanza maisha ya kujitegemea. Kama ilivyo kwa faru wengine alivunja ungo na kupandwa na faru wengine na kuzaa mtoto wake wa kwanza mwaka 1983. Mtoto wake huyu hakudumu sana maana alikufa mwaka 1989.
Pamoja na changamoto kadhaa Faru Vicky hakukata tamaa ya kuendeleza kizazi chake na alifanikiwa kuzaa watoto wengine wengi ndani ya hifadhi hiyo.
Utulivu, upole,maarifa na namna alivyokuwa makini katika kuchagua madume inadhihirisha kuwa chema chajiuza na kibaya chajitembeza.
