Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Timotheo Mnzava (Mb) leo tarehe 13 Machi, 2026 Karatu imedhihirishiwa kuwa Ngorongoro ni sehemu pekee duniani yenye ushahidi timilifu wa mwanzo wa binadamu wa kale.
Umwamba huo wa kihistoria ulioainishwa na wabobezi wa mambo kale umehifadhiwa katika makumbusho ya Urithi Geopark Museum iliyopo Karatu mkoani Arusha.
Akijinasibu mbele ya kamati ya bunge kuhusu ukweli huo Afisa Mhifadhi Mkuu wa mambo kale Dkt.Agness Gidna amesema muunganiko wa maisha ya binadamu kutoka zaidi ya miaka Milioni Mia tatu iliyopita hadi kizazi cha sasa inapatikana katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro.
Wabunge wa kamati hiyo wamefurahishwa na uwepo wa makumbusho hiyo ni kuitaka mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro kuendelea kutangaza makumbusho hiyo na kazi zake za kihistoria duniani.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Timotheo Mnzava ameishauri wizara ya Maliasili na Utalii kutanua wigo wa matangazo ya vivutio vya utalii ikiwemo makumbusho hiyo.
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) ameeleza Kamati hiyo kuwa Wizara na taasisi zake inaendelea mkakati wa kutangaza utalii kwa kupitia masoko mbalimbali ya kimkakati Ulaya, Asia, Amerika ili kufikia malengo ya Serikali na kufikia zaidi ya watalii milioni 8 ifikapo mwaka 2030 kw akuhakikisha kuwa kila mwaka bidhaa moja mpya inapelekwa sokoni.
Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi Ngorongoro Bw. Abdul-Razaq Badru amesema mikakati ya kuboresha eneo la makumbusho hiyo kwa kuongeza miundombinu mbalimbali ya kuvutia wageni wanaotembelea inaendelea ili kwenda sambamba na chapa ya Ngorongoro kama Premium Safari Destination.
