Na. Mwandishi wetu.
Askofu wa Kanisa la Victoria's Church lililopo Tabata Bima, Elias Chesa, amesisitiza kuwa amani ya kweli haiji kwa maneno matupu bali inatokana na injili ya amani inayohubiriwa na kuambatana na maombi ya dhati kwa ajili ya taifa.
Akirejea maandiko kutoka kitabu cha Wakolosai, Askofu Chesa ameeleza kuwa watumishi wa Mungu wana jukumu la kufanya dua, ishara, na maombi ili jamii iweze kuishi kwa utulivu na amani, kwani maombi hayo ndiyo yanayofungua milango ya utulivu wa kiroho na kimwili.
Alibainisha kuwa injili inayohubiriwa inalenga kuwafanya watu wajitambue na kuacha makosa yao, jambo ambalo ni hatua ya kwanza kuelekea amani ya kweli inayotoka kwa Mungu.
Katika kuelezea mchakato wa kupatikana kwa amani hiyo, kiongozi huyo wa kiroho amerejea kitabu cha Isaya akisema kuwa watumishi wa Mungu wanapaswa kupiga kelele bila kusita ili kuwakumbusha watu kutubu na kuacha matendo maovu yanayohatarisha usalama wa jamii.
Askofu Chesa amefafanua kuwa amani haiwezi kuwepo ikiwa watu hawafuati mapenzi ya Mungu au wanajihusisha na vitendo vya dhuluma na tamaa, akitolea mfano amri kumi zinazokataza kutamani mke au mali ya jirani.
Kwa mujibu wa Askofu huyo, amani inakuja pale watu wanapoacha kufanya vitendo vibaya vinavyovuruga utulivu, na hivyo watumishi wa Mungu wana nafasi kubwa ya kuendelea kuhubiri toba na injili ya amani ili kujenga taifa lenye mshikamano na uadilifu.
