Taasisi ya Benki ya Dunia inayojihusisha na utoaji mikopo na misaada kwenye sekta binafsi (International Finance Corporation (IFC), imeahidi kushirikiana na Serikali ya Tanzania kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo (DIRA 2050) kwa kuiwezesha sekta binafsi kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ya nishati na miundombinu ya reli.
Ahadi hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Taasisi hiyo, Bw. Ethiopis Tafara, alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumb wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, Makao Makuu ya Taasisi hiyo, pembezoni mwa Mikutano ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), jijini Washington D.C, nchini Marekani.
Aliipongeza Tanzania kwa kufungua fursa ya kuishirikisha sekta binafsi katika kutekeleza DIRA hiyo ikiwemo kufungua milango kwa sekta hiyo kuwekeza katika uzalishaji na usambazaji wa nishati ya umeme na bandari.
Bw. Tafara alisema kuwa IFC iko tayari kudhamini utekelezaji wa mradi wa Reli ya Kisasa-SGR kwa kujenga miundombinu itakayochochea na kukuza biashara katika ushoroba ambapo reli hiyo itapita kwa kuongeza thamani ya mradi huo mkubwa ili uweze kusafirisha bidhaa nyingi zaidi na kuwa na tija.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, alieleza jitihada mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji na kuialika IFC kushiriki katika utekelezaji wa DIRA 2050.
Mhe. Balozi Omar alisema kuwa Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuangalia mifumo ya kodi na vivutio vingine ili kuongeza kasi ya ushiriki wa Sekta binafsi katika maendeleo ya nchi pamoja na wananchi wake kwa ujumla kupitia ajira na ufanyaji biashara.
Kwa mujibu wa tathmini ya IFC ya mwaka 2025, taasisi hiyo imewekeza takribani dola milioni 197.4 katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026, kupitia mikopo ya muda mfupi iliyolenga kuchochea shughuli za sekta binafsi.
Aidha, kiasi cha uwekezaji wa IFC nchini Tanzania kimefikia dola milioni 315.9, ambapo asilimia 74 imeelekezwa katika sekta ya huduma za kifedha na asilimia 26 katika viwanda, kilimo-biashara, na huduma nyingine.
IFC pia inaunga mkono utekelezaji wa Mradi wa Usafiri wa Mabasi yaendayo Haraka (BRT) jijini Dar es Salaam kupitia huduma za ushauri wa PPP, pamoja na kutekeleza Mpango wa Kitaifa wa Jinsia (Gender Program) wenye thamani ya dola milioni 6.3 hadi mwaka 2028, unaolenga kuongeza ushiriki wa wanawake katika shughuli za kibiashara.
Mikutano hiyo ya uwili (bilateral meetings), imewashirikisha pia Waziri wa Nchi-Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, Dkt. Juma Malik Akil, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Mipango ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dkt. Tausi Kida, Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Dkt. Elsie Kanza, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Fedha na Mipango Zanzibar, Bw. Aboud Hassan Mwinyi, Kaimu Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Rished Bade, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, Msaidizi wa Katibu wa Baraza la Mawaziri, Bw. Francis Mossongo na maafisa wengine wa Serikali.
