Katika kipindi hiki ambacho taifa lipo kwenye kampeni kabambe ya kusaka maridhiano, amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa, sauti za vijana zimeanza kusikika zikihimiza matumizi ya diplomasia na mazungumzo badala ya vurugu.
Rajab Ali, kijana kutoka Kigamboni jijini Dar es Salaam, ametoa mwito kwa vijana wenzake wa kizazi cha sasa (Gen Z) kutoingia barabarani kutafuta suluhu ya changamoto zinazowakabili, akisisitiza kuwa njia ya maandamano na vurugu si suluhisho sahihi.
Akizungumza kwa uchungu kuhusu athari za machafuko, Rajab amekumbushia matukio ya nyuma ambapo maandamano yalisababisha watu kupoteza maisha na kuleta adha kubwa kwa wananchi, ikiwemo kupanda kwa bei ya bidhaa na hofu iliyowafanya watu washindwe kutoka nje kupata mahitaji yao ya msingi hata kama walikuwa na fedha.
Rajab amebainisha kuwa msukumo wa kuwataka vijana waandamane si jambo zuri na ni maamuzi yasiyo na tija kwa mustakabali wa nchi, kwani badala ya kutatua matatizo, maandamano huongeza changamoto na kurudisha nyuma juhudi za maendeleo.
Ameshauri kuwa ni vyema watu wakakaa chini na kujipanga vizuri kwa kuandaa mifumo rasmi ya kutatua changamoto zinazojitokeza kwa kutumia busara na mantiki. Kwa mujibu wa kijana huyo, ni muhimu kwa vijana kutotawaliwa na mihemko pale mambo yanapokwenda kinyume na matarajio yao, bali watafute suluhisho sahihi kwa kuwafuata viongozi na kueleza maoni yao kwa njia za amani na kistaarabu.
Msisitizo wa Rajab unakuja wakati ambapo mshikamano wa kitaifa unatajwa kuwa ndio nguzo kuu ya kulinda tunu za amani ambazo Tanzania imekuwa ikijivunia kwa miongo mingi.
Ameeleza kuwa kuwasikiliza viongozi na kutafuta njia bora ya kusuluhisha mambo ni hatua ya kishujaa zaidi kuliko kufanya vurugu ambazo mwisho wake ni maumivu kwa jamii nzima.
Rajab amewataka vijana wenzake kuwa mstari wa mbele katika kutunza amani iliyopo kwa kuelewa kuwa suluhu ya kudumu haipatikani barabarani kupitia vurugu, bali inapatikana kwenye meza ya mazungumzo ambapo hoja hupingwa kwa hoja na si kwa nguvu.
