TANGAZO

TANGAZO

HAYA NDIYO YALIYOBAINIWA NA TUME YA UCHUNGUZI WAKATI WA UCHAGUZI MKUU OKTOBA 2025 NA BAADA


 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, leo Aprili 23, 2026, amepokea ripoti ya Tume ya Rais iliyoundwa kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, katika hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Tume, Jaji Mstaafu Othman Chande, amesema:

“Yanayodaiwa kuwa maandamano hayakuzingatia matakwa ya Ibara ya 18 na 20 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) na sheria za nchi ikiwemo maandamano kuwa ya amani na kutoa notisi kwa Jeshi la Polisi kwa mujibu wa vifungu vya 42 na 43 vya Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma Saidizi.” 

“Haki ya kila mtu kushiriki uchaguzi kama mpiga kura au mgombea ni haki ya kikatiba kwa mujibu wa Ibara ya 5 ambayo haipaswi kupokwa.” 

“Ghasia zilipangwa na kutekelezwa siku iliyotangazwa kisheria kuwa ni siku ya Uchaguzi Mkuu. Hivyo, kufanya ghasia siku hiyo ilikuwa ni kupoka haki ya Kikatiba na Kisheria za wananchi wengine ikiwemo haki ya kupiga  na kupigiwa kura” 

“Washiriki wa ghasia za wakati  na baada ya Uchaguzi Mkuu walibeba silaha za aina mbalimbali zikiwemo mawe, nondo, mkuki, sururu, fimbo, marungu, visu, viberiti, vilipuzi, bunduki, manati, kombeo, rato na mapanga jambo ambalo haliruhusiwi kisheria katika maandamano ya amani.”

“Hii ni kinyume na sheria na taratibu za Kimataifa (Ibara ya 21 ya Mkataba wa Haki za Kiraia na Kisiasa, 1966), Kikanda (Ibara ya 11 ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Watu na Binadamu, 1981 na Ibara ya 10 na 11 ya Mkataba wa Ulaya wa Haki za Binadamu, 1950) na Kitaifa (Ibara ya 18 na 20 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977) haziruhusu maandamano ya watu waliobeba silaha; na;”

“Sheria na taratibu za Kimataifa, Kikanda na Kitaifa haziruhusu maandamano yanayosababisha taharuki katika jamii, kuhatarisha usalama wa Taifa, kusababisha uharibifu wa mali za umma na binafsi pamoja na kuhatarisha maisha ya watu wengine. Mambo hayo yakifanyika, yanakuwa kinyume cha tafsiri ya maandamano ya amani.”

“Kwa kuzingatia sheria na kanuni zinazotawala maandamano ya amani kimataifa, kikanda na kitaifa na ushahidi uliowasilishwa mbele ya Tume, ni maoni ya Tume kuwa kilichotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa tarehe 29 Oktoba, 2025 hakikuwa maandamano ya amani na hivyo kuwa nje ya kinga za sheria na kanuni hizo.”

"Waandamanaji walibeba silaha mbalimbali, isivyoruhusiwa katika maandamano ya amani".

"Sheria haziruhusu maandamano yanayosababisha taharuki katika jamii, kuhatarisha maisha ya watu wengine. Mambo hayo yalifanyika kinyume cha sheria na tafsiri ya maandamano ya amani"

“Tume imepata ushahidi usio na shaka kuwa matukio  ya ghasia za Oktoba 2025 yalipangwa, yaliratibiwa, yalifadhiliwa na kutekelezwa na watu waliopata mafunzo. Waratibu walitumia mbinu mbalimbali, ikiwemo kuwatumia watu wasio na ufahamu wa kina na vijana waliokata tamaa, huku wakihakikisha kuwa vitendo vya ghasia vinafanyika kwa wakati mmoja katika maeneo tofauti ili kuwachanganya na kuwatawanya Polisi.”

“Taarifa na ushahidi unathibitisha kuwa, kuna watu waliokuwa wakizunguka katika maeneo mbalimbali kama vile mitaani, vyuoni, kwenye masoko na stendi za mabasi wakishawishi na kuwaandikisha (recruit) watu mbalimbali kushiriki katika ghasia za wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu.”

“Mfano; watoto wanaoishi katika mazingira magumu, waendesha pikipiki (bodaboda) na wajasiriamali wadogo walieleza kuwa walipewa fedha kati ya sh. 10,000 hadi sh. 50,000 na waliahidiwa ajira na maisha bora.  Ilielezwa zaidi kuwa kuanzia tarehe 12 Oktoba, 2025 hadi 28 Oktoba, 2025 waliwekwa pamoja, kupewa mafunzo, kuandaliwa na kuhamasishwa kuwa sehemu ya kuanzisha na kushiriki ghasia siku ya Uchaguzi.”

“Aidha ilibainika kuwa, makundi yaliyoshawishiwa ndio walihusika zaidi kutekeleza ghasia, wakati wahusika wakuu wa ghasia na waratibu hawakuwepo kwenye maeneo ya matukio, hali iliyochangia kwa kiasi kikubwa kutokukamatwa kwao, huku wengi wa waliokamatwa wakiwa ni wananchi wa kawaida wakiwemo, wafuata mkumbo,  au kushawishiwa kwa malipo kidogo au ahadi za kunufaika na mabadiliko waliyoyapanga, bila kuwa na uelewa wa malengo halisi ya wahusika wakuu na waandaji.”

”Mbinu 16 zilizotumiwa na wahusika wakuu na waratibu kufanikisha ghasia za wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu. Baadhi ya mbinu hizo ni: kuweka vizuizi barabarani, kuchoma moto mali mbalimbali, matumizi ya ishara mbalimbali kutambuana, matumizi ya pikipiki kuanzisha ghasia, na uanzishaji wa ghasia sehemu nyingi kwa wakati mmoja.”

“Mfano; watoto wanaoishi katika mazingira magumu, waendesha pikipiki (bodaboda) na wajasiriamali wadogo walieleza kuwa walipewa fedha kati ya sh. 10,000 hadi sh. 50,000 na waliahidiwa ajira na maisha bora.  Ilielezwa zaidi kuwa kuanzia tarehe 12 Oktoba, 2025 hadi 28 Oktoba, 2025 waliwekwa pamoja, kupewa mafunzo, kuandaliwa na kuhamasishwa kuwa sehemu ya kuanzisha na kushiriki ghasia siku ya Uchaguzi.”  

“Kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa kwenye Tume, na maelezo niliyoyatoa hapo juu, matukio yale yalikuwa na malengo makuu yafuatayo:

(a) Kuzuia na/au Kuvuruga Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025

(b) Kufikisha Ujumbe kwa Serikali

(c) Wizi na Uporaji”

"Idadi ya vifo 518 inaweza kuwa siyo ya mwisho kwani baadhi ya watu au ndugu zao waliamua kwenda kutibiwa maeneo binafsi." 

“Tume pia ilipokea madai kutoka kwa waathirika na mashahidi wengine kuhusu watu kupigwa risasi, kujeruhiwa au kuuawa katika maeneo ambayo hayakuwa na ghasia au vurugu. Kuna madai ya watu kupigwa risasi  kwenye makazi yao ikiwa ni pamoja na ndani ya nyumba au sebuleni na ndani ya maduka. Hizo ni tuhuma nzito zinazoashiria uwezekano wa matumizi ya silaha za moto kinyume na miongozo na kanuni za kimataifa, kikanda na kitaifa kuhusu matumizi ya silaha hizo. Hili ni jambo jingine linalohitaji kufanyiwa upelelezi wa kina na wa kijinai.”