Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema Serikali itaendelea kuwaunga mkono wafanyabiashara ndogondogo nchini wakiwemo wasusi, waendesha bodaboda, mama lishe na baba lishe kwa kuwawezesha kupata mikopo yenye masharti nafuu inayotolewa katika halmashauri mbalimbali.
Mahundi ameyasema hayo alipohudhuria tamasha la “Urembo na Ibada” lililoandaliwa na mjasiriamali na mmiliki wa saluni, Maria Wilson maarufu kama Chido Point, jijini Dar es Salaam na kukutanisha zaidi ya wanawake 300 Aprili 03, 2026.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara ndogondogo ili wajikwamue kiuchumi.
“Niwasihi mfike kwenye halmashauri zenu kufuata utaratibu wa mikopo hiyo na kuchangamkia fursa zilizopo. Aidha, nikiwa Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Mbeya, nitaendelea kushirikiana na Chido Point katika kuandaa na kuratibu tamasha hili, linalotarajiwa kufanyika mwezi Julai mwaka huu mkoani Mbeya,” amesema Mahundi.
Kwa upande wake muandaaji wa tamasha hilo, Maria Wilson amesema lengo la tamasha hilo ni kuwaunganisha wasusi kutoka mikoa mbalimbali ili kubadilishana uzoefu na kukuza taaluma ya ususi nchini na ameishukuru Serikali pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii kwa kuendelea kuwajali wasusi, huku akiomba wizara nyingine ikiwemo Wizara ya Afya kuangalia ustawi wao hasa katika masuala ya afya na usalama kazini.
“Tamasha hili linalenga kuwaunganisha wasusi na kuwahamasisha wazazi kuwapa kipaumbele watoto wao wenye vipaji vya ususi waweze kujiajiri na kuchangia maendeleo ya taifa” amesema Maria Wilson.
Baadhi ya washiriki wa tamasha hilo wameeleza kufurahishwa na jukwaa hilo pamoja na juhudi za Serikali, wakisema limewapa maarifa na motisha ya kukuza biashara zao na elimu waliyoipata imewapa mbinu mpya zitakazowasaidia kuboresha kazi zao.




