TANGAZO

TANGAZO

Umuhimu wa Kulinda Amani ya Tanzania kwa Upendo na Mshikamano wa Kitaifa

 


Amani ni taswira ya utulivu wa moyo na mazingira yanayomfanya binadamu kutekeleza majukumu yake bila hofu wala wasiwasi wowote.

Kwa mujibu wa Adela Thomas, Afisa Msuluhishi wa Migogoro katika taasisi ya Peace Family wilayani Ubungo, amani ndiyo msingi wa furaha katika kila ngazi ya maisha kuanzia ngazi ya familia, maeneo ya kazi, hadi kufikia kiwango cha kitaifa. 

Anasema bila amani, hakuna furaha inayoweza kustawi, kwani amani ni kila kitu kinachogusa hisia za ndani za binadamu na kumpa uhuru wa kutembea na kuingiliana na wenzake pasipo shaka. 

Ni tunu ya kipekee ambayo Tanzania imejaliwa na Mwenyezi Mungu, ikiwa ni kitu cha thamani kubwa ambacho mataifa mengi yanahangaika kukitafuta bila mafanikio.

Tanzania inatazamwa kama taifa teule lenye utulivu wa kipekee kiasi cha kuvutia watu kutoka mataifa mbalimbali duniani. Wageni hawa anasema Adela, hawaji nchini kutafuta madini au utajiri pekee, bali wengi wao wanakimbilia Tanzania kufuata amani ambayo katika nchi zao haipo. 

Ni jambo la kusikitisha kuwa wakati mwingine Watanzania wanaichukulia amani hii kama kitu cha kawaida, huku wakisahau kuwa Mungu amewapendelea sana kulinganisha na nchi nyingine zinazoteseka na machafuko. 

Hivyo basi, ni wajibu wa kila mwananchi kuwa mlinzi wa amani hii kwa kuhakikisha kuwa viashiria vyote vya uvunjifu wa amani vinatolewa taarifa kwa haraka ili kuzuia uharibifu ambao unaweza kugharimu vizazi vingi.

Athari za kupoteza amani zinafananishwa na mti wa matunda uliokatwa, ambapo kuurejesha katika hali yake ya awali huchukua muda mrefu sana. 

"Mti ukishakatwa, unahitaji muda mrefu wa kuchipua, kumea matawi, na hatimaye kutoa matunda tena, na hata ukirejea, mara nyingi hauwezi kuwa imara na mzuri kama ule wa mwanzo., " anasema Adela.

Kwa mantiki hiyo, amani ikitoweka, majeraha yanayobaki katika jamii hayaponi kwa urahisi. Ni heri kuilinda amani iliyopo sasa kuliko kuanza kuhangaika kuitafuta ikiwa imeshapotea, kwani gharama yake ni kubwa na mchakato wa kuirudisha ni wa maumivu makubwa na majuto.

"Amani ya kweli haipatikani kwa maneno matupu au kwa kuizungumzia tu, bali inajengwa kupitia umoja, upendo, na mshikamano wa dhati kati ya wananchi. 

"Ikiwa jamii itatengana na kila mtu kufuata njia yake bila kujali mwingine, uwezo wa kutunza amani utatoweka. " anasisitiza Adela.

Amesema Watanzania wanapaswa kuipenda nchi yao na kujivunia utambulisho wao wa amani kwa kutatua migogoro kwa njia ya mazungumzo na utulivu. 

Kwa kuendeleza umoja na mshikamano, taifa litaendelea kuwa kimbilio la wengine na mfano wa kuigwa duniani, huku kila mwananchi akishiriki kikamilifu kuilinda tunu hii ambayo ni nguzo kuu ya maendeleo na furaha ya binadamu.