TANGAZO

TANGAZO

WAZIRI MKUU AKAGUA MAENDELEO YA UJENZI WA UWANJA WA AFCON – ARUSHA





 Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, leo Ijumaa Aprili 17, 2026, amekagua maendeleo ya ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu unaojengwa jijini Arusha na kumuagiza mkandarasi ahakikishe mradi huo unakamilika kwa wakati.

Ujenzi wa uwanja huo unaojengwa katika kata ya Olomoti, Jijini Arusha ni sehemu ya maandalizi ya Mashindano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, yakayofanyika kwenye nchi tatu za Tanzania, Kenya na Uganda.

Akizungumza baada ya kupokea taarifa ya ujenzi wa uwanja huo, Waziri Mkuu amemuagiza mkandarasi wa mradi huo kuhakikisha kuwa ujenzi unakamilika kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.

Amesema “Katika kukuza sekta ya michezo, kuboresha afya za wananchi, pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia michezo. Mhe. Rais Dkt. Samia amefanya mengi likiwemo hili la kimichezo tusimwangushe kwa kufanya chini ya uwezo, natoa agizo kwa mkandarasi kuhakikisha unafanikisha zoezi hili la ukamilifu wa uwanja huu ndani ya muda na kwa kuzingatia ubora, viwango vya kimataifa kwa mujibu wa CAF.”

Amesisitiza kuwa maandalizi ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano ya AFCON 2027 ni heshima kubwa kwa Taifa, hivyo kunahitajika juhudi za ziada kuhakikisha miundombinu yote inakamilika kwa ubora unaotakiwa.

Mheshimiwa Waziri Mkuu ameendelea kuwasisitiza wakandarasi wote nchini kulipa wafanyakazi baada ya wao kuwa wamelipwa na Serikali fedha zao. “Kumekuwepo na tabia ya baadhi ya wakandarasi katika maeneo mbalimbali kutokuwalipa mafundi na vibarua kwa wakati.”

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutenga rasilimali za kutosha katika utekelezaji wa mradi huo.

Amesema uwanja huo ni miongoni mwa viwanja vya kisasa barani Afrika vilivyobuniwa kwa kuzingatia utambulisho wa kiutamaduni wa eneo husika na usanifu wake unaakisi alama muhimu za Taifa, ikiwemo Mlima Kilimanjaro, urithi wa jamii ya Kimaasai, pamoja na rasilimali ya madini ya Tanzanite. “Mfumo wa taa za uwanja huo umebuniwa kwa kuzingatia alama za utamaduni na utaifa wa Tanzania.”

Sambamba na ujenzi wa uwanja huo, Serikali inaendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa barabara tatu za njia nne zinazozunguka eneo la uwanja huo, kwa lengo la kuboresha miundombinu ya usafiri na kupunguza msongamano wa magari na watu wakati wa matukio mbalimbali, hususan siku za michezo. Mradi huo wa barabara unatekelezwa na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI kwa gharama ya takribani shilingi bilioni 20.

Uwanja huo, utakapokamilika, utakuwa na uwezo wa kuchukua jumla ya watazamaji 32,000. Ambapo hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 78, na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Julai 2026. Kwa mujibu wa tarifa ya mradi huo.