Uwezo wa taasisi za serikali kufanya kazi kwa ufanisi katika mazingira ya dharura hutegemea maandalizi ya awali na uwekezaji wa muda mrefu katika miundombinu na rasilimaliwatu.
Ripoti ya Tume ya Kuchunguza Matukio Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 imebainisha kuwa, uwezo wa taifa kuhimili dharura kubwa ya kibinadamu ulichochewa na uimarishaji wa sekta muhimu kama afya na ulinzi uliofanywa kabla ya janga kutokea.
Hii inadhihirisha kuwa taasisi hazipaswi kufanya kazi kwa ukadiriaji au kusubiri majanga yatokee, bali zinapaswa kuwa na mifumo imara inayoweza kuitika haraka wakati wa shinikizo kubwa.
Katika kipindi hicho cha ghasia, sekta ya afya nchini ilikabiliana na mtihani mzito kutokana na idadi kubwa ya majeruhi 2,390 waliohitaji matibabu ya haraka katika vituo vya umma na binafsi.
Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Chande Othman, alibainisha kuwa uwekezaji mkubwa ambao serikali imefanya katika kuboresha sekta ya afya ulikuwa mhimili mkuu wa kuokoa maisha.
Maandalizi haya yalisaidia hospitali na vituo vya afya kubeba mzigo mkubwa wa majeruhi katika mazingira ya dharura bila mfumo mzima wa huduma kuporomoka.
Umuhimu wa taasisi kujipanga muda wote pia ulijitokeza kupitia ushirikiano wa kitaalamu wa nyanja mbalimbali kama vile wataalamu wa vinasaba, picha, na saikolojia walioisaidia tume kuelewa masuala mahususi ya kijamii na kiuchumi yaliyotokana na ghasia hizo.
Hata pale vyombo vya usalama vilipokabiliana na hali ya mtawanyiko wa vurugu ambayo hawakuwa wameitarajia kikamilifu, uwepo wa mfumo imara wa mawasiliano na utayari wa kitaasisi ulisaidia kurejesha utulivu.
Kazi zilizofanywa na Ulinzi na watu wa Afya zimeinatoa somo kuwa nguvu ya taifa wakati wa dharura inategemea uimara wa taasisi zake kufanya kazi kwa pamoja na kwa mpango maalum badala ya matendo ya kushtukiza.
