MKUU wa Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Tanzania (TPTC), Brigedia Jenerali George Itang’are amesema kuwa kozi maalum ya Wanawake katika masuala ya ulinzi na usalama inalenga kuongeza ushiriki wa wanawake kikamilifu katika oparesheni za kulinda amani na kutatua migogoro kwa njia yenye tija na kuleta matokeo chanya.
Brigedia Jenerali Itang’are ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akifungua kozi hiyo inayofanyika katika kampasi ya TPTC iliyopo Kuduchi inayofadhiliwa na serikali ya Japan kwa ushirikiano na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) na Shirika la Umoja Mataifa linaloshughulika na Wanawake (UN Women).
Amesema mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za serikali na taasisi za ulinzi na usalama kuhakikisha wanawake wanapata nafasi kubwa zaidi katika shughuli za ulinzi wa amani ndani na nje ya nchi.
Brigedia Jenerali Itang’are amesema JWTZ limekuwa likitoa maelekezo mara kwa mara yanayohimiza ushiriki wa wanawake katika operesheni mbalimbali za kulinda amani, huku mafunzo hayo yakiwa miongoni mwa programu zinazotekelezwa kufanikisha lengo hilo.
“Lengo si kuongeza idadi ya wanawake pekee, bali kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika shughuli za amani na usalama. Tunahitaji ushiriki wenye matokeo, si takwimu tu,” alisema Itang’are
Alieleza kuwa mbali na mafunzo hayo, kuna programu nyingine zinazolenga kuwaandaa wanawake kwa nafasi za uongozi pamoja na kozi zinazohusisha masuala ya kijinsia ndani ya vyombo vya ulinzi na usalama.
Kwa mujibu wake, mafunzo hayo yanawakutanisha maofisa kutoka taasisi mbalimbali ikiwemo JWTZ, Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji na Jeshi la Magereza, hatua inayolenga kuimarisha ushirikiano miongoni mwa vyombo vinavyoshiriki katika operesheni za kulinda amani.
“Ulinzi wa amani unahusisha taasisi nyingi. Tunapokutana katika mafunzo kama haya tunajenga mahusiano mazuri ya kikazi na kuongeza uelewa wa pamoja kuhusu namna ya kutekeleza majukumu yetu katika misheni za amani,” aliongeza.
Aidha, alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoongoza katika kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika shughuli za ujenzi wa amani na operesheni za Umoja wa Mataifa, huku wanawake wa Kitanzania wakishiriki katika misheni mbalimbali za kimataifa.
Alibainisha kuwa kwa sasa baadhi ya nafasi za juu katika misheni za Umoja wa Mataifa zinazowakilishwa na Tanzania zinashikiliwa na wanawake, jambo linaloonesha dhamira ya nchi katika kukuza usawa wa kijinsia ndani ya sekta ya ulinzi na usalama.
Kuhusu washiriki wa mafunzo hayo, alisema jumla ya watu 30 wanashiriki, wakiwemo wanawake na wanaume, akifafanua kuwa ajenda ya wanawake, amani na usalama haiwahusu wanawake pekee bali inahitaji ushiriki wa kila mmoja katika kuhakikisha wanawake wanapata nafasi stahiki.
“Wanaume waliopo hapa ni sehemu ya utekelezaji wa ajenda hii. Jukumu lao ni kuhakikisha popote wanapokuwa wanahamasisha na kusimamia ushiriki wa wanawake katika masuala ya amani na usalama,” alisema.
Naye Balozi Mdogo wa Japan nchini Tanzania, Shoichi Ueda amesisitiza umuhimu wa kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za ulinzi wa amani, kuzuia migogoro na kurejesha hali ya kawaida baada ya migogoro, ikieleza kuwa ushirikishwaji huo ni msingi wa amani ya kudumu na maendeleo endelevu ya jamii.
Hata hivyo alisema Japan inathamini ushirikiano unaoendelea kati ya TPTC na wadau mbalimbali wakiwemo UNDP na UN Women, ambao wamekuwa wakichangia mafanikio ya programu hizo kupitia utaalamu na msaada wao.
Kwa mujibu wa Ueda , TPTC imejijengea sifa kama taasisi muhimu ya mafunzo ya kitaalamu ya ulinzi wa amani katika ukanda huu wa Afrika, huku kozi zinazowakutanisha washiriki kutoka Tanzania na nchi nyingine wanachama wa SADC zikitoa jukwaa muhimu la kujifunza, kushirikiana na kubadilishana uzoefu miongoni mwa wataalamu wa amani wenye taaluma na uzoefu tofauti.
Alieleza kuwa katika mazingira ya sasa ya usalama duniani ambayo yanazidi kuwa changamani, mahitaji ya watumishi wa kiraia na wale wa vyombo vya ulinzi na usalama walioandaliwa vizuri kwa ajili ya operesheni za kulinda amani yameongezeka zaidi kuliko wakati mwingine wowote.
“Migogoro na majanga ya kibinadamu yanaendelea kuathiri maeneo mengi duniani, jambo linalofanya ushirikiano wa kimataifa na juhudi za kuzuia migogoro kuwa muhimu sana. Japan inaamini kuwa kuimarisha uwezo wa taasisi kama TPTC kunachangia moja kwa moja amani na usalama wa kikanda na kimataifa,” alisema.
Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa UN Women nchini, Katherine Gufford alisema mafunzo hayo yanafanyika katika kipindi muhimu duniani ambapo Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Walinda Amani wa Umoja wa Mataifa mwaka 2026 kwa kaulimbiu ya “Wekeza katika Amani”.
Kwa mujibu wa Gufford amesema kuwekeza kwa wanawake walinda amani ni kuwekeza katika operesheni zenye nguvu zaidi, juhudi za kujenga amani zinazowajumuisha watu wote pamoja na jamii zinazostahimili changamoto mbalimbali.
Mwakilishi huyo alieleza kuwa wanawake walinda amani wana mchango mkubwa katika kuzuia migogoro, kulinda raia, kushirikiana na jamii, upatanishi pamoja na shughuli za kurejesha hali ya kawaida baada ya migogoro.
Alibainisha kuwa uzoefu na mchango wao huongeza ufanisi wa operesheni na kujenga imani kwa jamii zilizoathiriwa na migogoro.
Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa UN Women nchini, Katherine Gufford alisema kwa UN Women mafunzo hayo si tu fursa ya kukuza taaluma za washiriki, bali ni uwekezaji katika uongozi, ubora wa utendaji kazi na mustakabali wa taasisi za amani na usalama nchini Tanzania na kwingineko.
Alisema kuwa Umoja wa Mataifa kupitia UN Women utaendelea kuunga mkono ajenda ya wanawake, amani na usalama kwa kutoa msaada wa kisera, kuimarisha uwezo wa taasisi, kufanya tafiti na kujenga ushirikiano na serikali pamoja na taasisi za usalama.
Naye Msaidizi Mkuu Kitengo cha Utawala UNDP, Fridah Mwakasyoka alisema mwaka jana walifanya kozi hiyo vizuri na Chuo, wakapata fedha za ziada za kuendeleza mafunzo kama haya na kwamba mwaka huu ni awamu ya pili na wamefanya maboresho kidogo katika mtaala wa mafunzo haya ili kuyafanya yaendane na uhalisia wa maisha hasa masuala ya ulinzi.
“Moja wapo ya maboresho ni kuyafanya mafunzo haya kuwa jumuishi kwa kuwaweka wanaume kidogo tofauti na mwaka jana walihudhuria wanawake pekee. Kuna tofauti katika kuelezea mambo ya wanawake hauwezi kuwaacha wanaume nyuma hivyo ni vema kuwaweka pamoja na kuongea lugha moja,” alisema

