Katika mazungumzo ya kina yaliyofanyika kwenye kipindi cha Hot Zone kinachoendeshwa na Kasaco Media, mwandishi mwandamizi mstaafu Beda Msimbe ametoa mtazamo chanya kuhusu Ripoti ya Jaji Chande akibainisha kuwa ameipokea kwa mikono miwili kama hatua ya kwanza na muhimu ya kuanza kutibu majeraha ya Watanzania.
Msimbe amefafanua kuwa binadamu anapopita katika vipindi vigumu na mahangaiko makubwa, ni lazima apatikane mwanzo wa kuanzia ili kuweka msingi wa kutatua matatizo yaliyopo, na kwake yeye ripoti hiyo inawakilisha kielelezo hicho cha mwanzo wa mabadiliko.
Amesisitiza kuwa uamuzi wa kuifanya ripoti hiyo ijulikane kwa umma ni ishara ya uwazi, akijenga hoja kuwa Rais Samia Suluhu Hassan alikuwa na uwezo wa kisheria wa kutoitoa ripoti hiyo kama ambavyo ripoti nyingine nyingi za Rais hubaki kuwa siri, lakini uamuzi wake na muhtasari alioutoa Jaji Chande unawezesha jamii kufikiria na kujadili mustakabali wao.
Akielezea uzito wa ripoti hiyo kwa lugha ya picha, Msimbe amelinganisha hatua hiyo na mchakato wa kusafisha kisima cha maji, ambapo mara nyingi unahitaji kuyaondoa maji machafu ya mwanzo na kuyaacha mengine yatue kabla ya kupata maji safi ya kutumia.
Amesema kuwa ripoti hii kwake ni kama sehemu ya mwanzo ya kutibua hali ambayo si sahihi ili kuruhusu ukweli na haki vijichuje na hatimaye Taifa lipate suluhu ya kudumu baada ya "kuyachekecha" mambo yaliyojiri.
Kwa mujibu wa mwanahabari huyo mkongwe, hata katika ngazi ya familia, binadamu anapoharibikiwa ni lazima atafute mahali pa kuanzia kujitibu, na hivyo ripoti ya Jaji Chande imeweka mazingira muhimu kwa Watanzania kutathmini mambo muhimu yaliyotokea bila kuharibu utaratibu uliokusudiwa wa kuleta utulivu na maridhiano nchini.
